MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), amechafua hali ya hewa bungeni kwa kuitaka Serikali kuwachukuliwa hatua viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Mbunge huyo alisema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa, wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa madai ya kusababisha mauaji ya raia. Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bara, alisema katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi ilipotoka kwenye uchaguzi, viongozi hao wamekuwa wakihamasisha maandamano na kusababisha umwagaji wa damu za Watanzania. “Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi yetu ilipomaliza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Mbowe na Dk. Slaa wamekuwa wakitoa kauli za wazi na hata kusababisha mauaji ya watu bila hatia. “Kutokana na hali hii, sijui Serikali inafanya nini katika kuwachukulia hatua, kwani viongozi hawa wamekuwa wakitafuta umaarufu wa kisiasa kwa kuch...