WABUNGE WATAKA MBIO ZA MWENGE WA UHURU ZIFUTWE
MBIO za Mwenge wa Uhuru nusura ziahirishe shughuli za Bunge baada ya baadhi ya wabunge kutaka zifutwe na hoja hiyo ijadiliwe bungeni. Hata hivyo, suala hilo liligeuka shubiri kwa Waziri wa Nchi, Ofisa ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, kuzomewa na kurushiwa maneno ya kejeli alipojaribu kuzitetea mbio hizo. Chanzo cha mzozo huo kilitokana na maswali ya mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), aliyeihoji serikali kama kuna uwezekano wa kutoukimbiza Mwenge katika maeneo ya watu wasiouhitaji. Nyerere alisema watu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, hawautaki Mwenge huo kwa sababu unachochea uhasama, chuki na upotevu wa rasilimali. “Wakati wa mbio za Mwenge Musoma Mjini walilazimisha kuchukua magari ya halmashauri likiwemo la wagonjwa... huduma za afya zilisimama na hivyo kuleta chuki badala ya mwanga,” alidai. Nyerere pia alitaka kujua nini faida za mbio hizo, bajeti yake ni kiasi gani kwa mwaka na ...