Waziri wa Fedha, William Mgimwa, amesisitiza uamuzi wa Serikali kuendelea kutoza Sh 1,000 kwa kila mwezi kwa laini ya simu, licha ya kampuni za simu na wanasiasa kupinga. Akizungumza na mwandishi juzi, Mgimwa alikumbusha wanaolalamikia kodi hiyo, kwamba suala la ulipaji kodi kwa taasisi au watu binafsi, ni la kisheria kulingana na mapato yao na hali halisi iliyopo. Pia alieleza kushangazwa na matangazo ya baadhi ya kampuni kuhusu utozwaji kodi wananchi akisema wananchi ndio wanataka barabara, maji na umeme vijijini na kodi hizo zinakwenda kutumika huko. Kwa mujibu wa Mgimwa, kodi ya laini za simu na ya intaneti, imetengwa ikatumike kusaidia maji na uwezo wa Serikali kupeleka elimu vijijini jambo ambalo ni la maendeleo. "Wananchi wenyewe wanalalamikia ukosefu wa huduma na baada ya Serikali kupitia na kufanyia kazi changamoto hizo, imeridhia kodi hizo wanakuja watu wanalalamika," alisema. Alisisitiza kuwa ongezeko la kodi kwa huduma za ...