Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Askofu Mkuu Pietro Parolin . Suala la mapadri wa Kanisa Katoliki kuoa au la, limeibuka upya na tayari limeanza kuzua mijadala mikali duniani. Mjadala wa sasa umeibuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Askofu Mkuu Pietro Parolin ambaye aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo aliposema useja, yaani maisha ya utumishi ndani ya kanisa bila ndoa siyo imani, bali utamaduni na mazoea. Akizungumzia kauli hiyo, Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi alisema kauli ya Askofu Parolin haipingani na mafundisho ya kanisa. Askofu Mkuu Parolin ambaye aliteuliwa karibuni na Papa Francis kushika wadhifa huo kutoka kwa Kardinali Tarcisio Bertone amenukuliwa na Gazeti la El Universal la Venezuela, Amerika ya Kati akieleza kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa.