LUDWIGNCHEMBA ATAKA MBOWE NA DR. SLAA WAKAMATWE KWA MAUAJI YA RAIA
Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bara, alisema katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi ilipotoka kwenye uchaguzi, viongozi hao wamekuwa wakihamasisha maandamano na kusababisha umwagaji wa damu za Watanzania.
“Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi yetu ilipomaliza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Mbowe na Dk. Slaa wamekuwa wakitoa kauli za wazi na hata kusababisha mauaji ya watu bila hatia.
“Kutokana na hali hii, sijui Serikali inafanya nini katika kuwachukulia hatua, kwani viongozi hawa wamekuwa wakitafuta umaarufu wa kisiasa kwa kuchochea chuki na mauaji dhidi ya raia.
“Kwa hali hiyo, tangu kipindi hicho hadi leo hii wanasubiri nini badala ya kwenda kuwaweka jela, kwani huko ndiko wanatakiwa kuwa,” alisema.
Mwigulu, alisema kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya viongozi wa siasa, ambao wamekuwa wakitumia majukwaa na kuhubiri umwagaji damu ni hatari kwa taifa.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakitumia majukwaa hayo na kusababisha vifo vya wananchi, huku akitaja vurugu zilizotokea katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Arusha na Singida.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alisema Serikali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi na kwamba mahakama ndicho chombo chenye uamuzi wa mwisho dhidi ya adhabu kwa raia au kiongozi yeyote wa kisiasa.
Kauli hiyo ya Mwigulu ilionekana kuchafua hali ya hewa ndani ya Bunge, ambapo Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo wa Spika, huku akimtaka Mwigulu kuthibitisha kauli yake, vinginevyo aombe radhi.
Wenje alisema hoja ya Mwigulu imekosa mashiko na ina lengo la kuwadhalilisha viongozi wa Chadema, huku akisahau kuwa baada ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki, aliyekuwa Mwenyetiki wa Chadema tawi la Usa River, Omari Mbwambo, aliuawa na watu anaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kwa wanasiasa wanaokiuka maadili na kusababisha uvunjifu wa amani.
“Wanataaluma kama vile madaktari, wahandisi, wahasibu na hata wakandarasi pindi wanapokiuka maadili ya kazi zao huchukuliwa hatua kwa kufutiwa leseni zao.
“Vile vile viongozi wa kisiasa wanayo maadili yanayowaongoza, kwanini pale wanapokiuka maadili ya kazi zao hawachukuliwi hatua kama ilivyo katika makundi hayo? (taaluma),” alisema Kilango
Comments
Post a Comment