Unajua athari za kuitana sweet, dear, baby...?
Mbali na hilo, yapo maneno mengine kama sweet, dear, honey na mengine mengi. Maneno yote hayo ya Kiingereza, yana maana zaidi ya moja, lakini kubwa zaidi ni kumaanisha mpenzi, mpendwa (hutumika katika kuonesha mapenzi ya dhati kwa mwingine).
Leo nataka kukupa kitu kipya kabisa kichwani mwako. Unahitaji utulivu wa hali ya juu ili kujifunza hili. Ni maneno mazuri sana, ya kipekee lakini kwa upande mwingine ni hatari kwa sababu hukaribisha matatizo ambayo hayakutarajiwa na mtumiaji.
HUTUMIKA WAPI HASA?
“Dear, naomba uniamshe saa 12:00 asubuhi, kesho nina vikao vingi sana asubuhi,” inaweza kuwa kauli ya mume akimwambia mkewe, ambaye naye anamjibu: “Sawa sweet, usijali.”
Kwa hakika ndipo sehemu sahihi zaidi kutumika. Ni maneno yenye mshawasha mkubwa na huonesha penzi la dhati lililopo moyoni mwa mhusika kwenda kwa mpenzi wake.
Husisimua na kuongeza ladha ya mapenzi ya kweli. Kumuita mpenzi wako kwa majina ya kimapenzi huongeza zaidi upendo na msisimko wa moyo. Mwenzi hujiona wa kipekee na mapenzi huzidi kukua.
Kwa maana hiyo basi, ni sahihi zaidi kwa wapenzi kuitana majina niliyotaja hapo juu na mengine yanayofanana na hayo kwa lugha yoyote ile, ila iwe inatambulika vizuri na anayetamkiwa.
ATHARI SASA!
Kwa upande mwingine kuna athari za kutumia maneno hayo. Zama hizi, maneno hayo yanaonekana ya kawaida tu. Mtu yeyote anaweza kumuita yeyote mpenzi, honey, baby n.k. Hapo ndipo kwenye tatizo lenyewe.
Kwa ujumla wanawake ndiyo wanaongoza zaidi kuitana majina hayo. Wakati mwingine huenda mbali zaidi na kuwaita hata wanaume majina hayo ya kimapenzi. Si rahisi kuona athari zake kwa haraka na moja kwa moja, lakini zipo na wengi zimewasababishia matatizo. Ngoja tuone..
HUPUNGUZA THAMANI
Kama nilivyotangulia kusema awali, maneno
niliyotaja hapo juu husisimua na kuongeza mapenzi. Kwa kuyatumia vinginevyo, basi kwa kiasi kikubwa huanza kukuathiri na kupunguza thamani ya neno lenyewe.
Kama unaweza kumwita mfanyakazi mwenzako dear, mtu wa jinsi sawa na wewe sweet ni wazi hata utakapomuita mpenzi wako au wewe kuitwa na yeye, halitakuwa na nguvu sana ya mapenzi kwa sababu ni neno ulilolizoea kila wakati.
HUKARIBISHA USALITI
Wakati mwingine unaweza kujikuta umeingia kwenye usaliti bila kutarajia. Veronica, mfanyakazi wa saluni moja ya kiume iliyopo Sinza, Dar alitoa ushuhuda ufuatao:
“Mimi naishi na mchumba wangu, tuna mtoto mmoja mwenye miaka mitatu. Nafanya kazi saluni. Tangu nimeanza hii kazi, nimejifunza kutumia maneno matamu ya kumfurahisha mteja na wakati mwingine kumfanya akupe tipu baada ya kumaliza kazi.
“Kuna kaka mmoja nilizoeana naye sana. Kama kawaida, huwa namkaribisha kwa kumuita dear au sweet. Wakati nikiendelea kumfanyia scrub, mazungumzo yetu hutawaliwa na dear, sweet, nikajikuta nimezidi kumzoea.
“Kwa sababu tulibadilishana namba, mara akaanza kuwa na mazoea ya kunitumia meseji, akija ananipa pesa, anaondoka. Mazoea yakazidi. Nikajikuta nimemzoea na kuna siku ambayo siwezi kuisahau kabisa.
“Ni siku niliyomsaliti mchumba wangu...mbaya zaidi na huyo jamaa naye ana mke wake. Niliumia sana, lakini naamini kama nisingekuwa na mazoea ya kumuita majina ya kimapenzi nadhani nisingeingia mtegoni. Moyo wangu unauma sana, najuta kumsaliti mpenzi wangu.”
Unaweza usione athari hii moja kwa moja, lakini ndugu zangu chukua jambo hili leo; wanaume wengi wakiitwa kwa majina ya kimapenzi husisimka sana – hujiona wenye bahati na mara hushawishika kuingia mapenzi.
Kama mwanamke hatakuwa makini atajikuta ametumbukia. Ya nini yote hayo, wakati unaweza kubadilisha mazoea hayo?
ANGALIA TOFAUTI
Rafiki zangu, kati ya maneno niliyoyataja, kuna ambayo yanakubalika kutumiwa na wasio na uhusiano lakini wawe na undugu wa damu. Mathalani baba, mama, kaka, dada, shangazi nk.
Hakuna tatizo kumuita mtu mpendwa, lakini siyo baby, sweet, mpenzi na mengine yenye maana ya moja kwa moja ya kimapenzi. Umenipata? Akili za kuambiwa, changanya na zako kisha unazifanyia kazi! Chukua kinachokufaa!
Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine. Wewe ni muhimu sana kwangu. Bye!samwelmlawa.blogspot.com
Comments
Post a Comment