PENZI LISILO ISHA 4


Jafet, kijana mdogo ambaye amehitimu darasa la saba na kufaulu vizuri kuendelea na masomo ya sekondari, anajikuta akikwama kuendelea na shule kutokana na ufukara wa kupindukia wa wazazi wake. Hali hiyo inamuumiza sana hasa anapoona wenzake wameanza kwenda shule, muda wote anashinda akiwa analia na kujiinamia kwa huzuni.
Mama yake aliyekuwa akijishughulisha na kazi ya kufanya vibarua vya kupalilia mashamba ya mihogo ili apate chakula cha yeye na familia yake, naye anaumizwa sana na hali aliyokuwa nayo mwanaye. Baada ya kumlalamikia na kumlilia sana, mwanamke huyo maskini anaamua kumsaidia mwanaye.
Kama miujiza, anapata habari za mapadri waliokuwa wanasaidia kuwasomesha watoto waliofaulu kutoka kwenye familia za kimaskini. Hatimaye ndoto ya Jafet ya kuendelea na masomo iliyokuwa imefifia, inang’ara upya baada ya mapadri kukubali kumsomesha. Anapelekwa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kwimba, Mwanza anakoyaanza masomo.
Siku zinasonga mbele, Jafet anaanza kubadilikia kimwili na kuwa mkubwa. Ni katika kipindi hicho ndipo anapoanza kusumbuliwa na hisia za kimapenzi na kutamani kuwa na msichana. Anaanza kujenga mazoea na msichana mmoja, Anna aliyekuwa akisoma shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru.
Anapata nafasi ya kuzungumza na msichana huyo ambapo anamueleza hisia alizonazo ndani ya moyo wake lakini anashindwa kumpa majibu baada ya baba mzazi wa msichana huyo kumpigia simu mwanaye. Siku chache baadaye, msichana huyo anamtumia Jafet barua na kadi yenye ujumbe wa mapenzi.
Je, nini kitafuatia?
Baada ya kukabidhiwa bahasha ya khaki na karani wa shule, Jafet hakwenda tena darasani, badala yake alienda moja kwa moja bwenini na alipoingia tu
, aliifungua bahasha hiyo kwa umakini. Akakutana na bahasha nyingine ndani iliyokuwa na mauamaua mazuri, akaitoa na kuifungua.
Alichokiona kilimfanya asiyaamini macho yake, kulikuwa na kadi nzuri iliyokuwa imepuliziwa manukato mazuri, akaitoa huku uso wake ukiwa umejawa na tabasamu na kuifungua ndani.Alichokutana nacho kilimfanya apigwe na butwaa iliyochanganyikana na furaha ya ajabu. Kulikuwa na ujumbe mzuri wa kimapenzi ulioandikwa kwa mwandiko nadhifu wa kike, kutoka kwa Anna akimueleza kwamba amekubali ombi lake la kumtaka wawe wapenzi.
“Tangu siku ya kwanza nilipokuona, nilijikuta moyo wangu ukipigwa na ganzi ya mapenzi juu yako, nikatokea kukupenda sana ingawa nilishindwa kukukabili na kukueleza ukweli.“Kama ungechelewa kidogo huenda mimi ndiyo ningekuanza, siku zote nilikuwa naogopa kukwambia nikihisi utaniona kama sijatulia.
“Nakupenda sana Jafet na naomba ukipata muda, nipigie simu kwa hii namba yangu lakini piga muda wa usiku kwa sababu hapa shuleni haturuhusiwi kuwa na simu.Ndimi nikupendaye kwa dhati, kutoka ndani ya moyo wangu, Anna.”
Jafet alirudia kuusoma ujumbe huo zaidi ya mara tatu, akaanza kurukaruka kwa furaha ndani ya chumba hicho huku akilitaja jina la Anna. Alijikuta akiwa na furaha ya ajabu ndani ya moyo wake, akaendelea kuchekacheka mwenyewe kama mwendawazimu huku taswira ya msichana huyo mrembo ikiendelea kupita ndani ya kichwa chake.
“Lakini yeye ni tajiri sana na mimi ni maskini, nikimwambia ukweli wa maisha yangu si ndiyo utakuwa mwisho wa mapenzi yetu?” furaha ya Jafet iliingia doa baada ya kuanza kufikiria tofauti kubwa iliyokuwepo kati yake na msichana huyo.
Japokuwa hakupata muda wa kuzungumza naye kuhusu familia zao, kwa alichokiona kule mjini alipokutana na msichana huyo, kilitosha kumpa mwanga kwamba hakuwa akitoka kwenye familia ya kawaida kama alivyodhani awali.
Hata hivyo, kwa kuwa msichana huyo alikuwa amemuandikia namba ya simu chini ya ujumbe ule mzuri wa mapenzi aliomtumia, alijipa kazi ya kuhakikisha anatafuta simu kwa udi na uvumba kwa wanafunzi wenzake ili ampigie na kuzungumza naye.
Kutokana na sheria kali zilizokuwepo kwenye shule hiyo aliyokuwa anasoma, hakuna mwanafunzi aliyekuwa anaruhusiwa kuwa na simu na yeyote aliyekutwa nayo, adhabu kali zilikuwa zikitolewa, jambo lililosababisha hata wale wachache waliokuwa nazo kuzificha sana.
Maadili makali ya kidini yaliyokuwepo shuleni hapo, yalikuwa yakiwalazimisha wanafunzi wote kuwa watiifu, kumwogopa Mungu na kutii sheria na mamlaka zilizowekwa, jambo lililotajwa kuwa msingi wa mafunzo ya upadri ambayo wanafunzi wote waliokuwa wakipitia shule hiyo, walikuwa wakitakiwa kuyapata kama ulivyo mkataba ambao kila mwanafunzi anatakiwa kuujaza pindi anapoanza shule.
Baada ya kuhangaika sana bila mafanikio kupata mtu mwenye simu, Jafet alijiwekea nadhiri ndani ya moyo wake kwamba siku atakayotumwa tena mjini kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya miradi shuleni hapo, atatafuta kibanda cha simu ili azungumze na Anna kwa kina.
Siku hiyo ilipita huku Jafet akionesha kukolezwa vibayana penzi la msichanamrembo Anna, kila alipokuwa akimfikiria, hata kama alikuwa yupo katikati ya kipindi, mwalimu akiendelea kufundisha, akili zake zilikuwa zikihama kabisa na kuanza kumfikiria msichana huyo mrembo.
“Lazima nikuoe, lazima uwe mama wa watoto wangu Anna,” Jafet alijikuta akiropoka bila kujua kwamba mwanafunzi mwenzake aliyekuwa amekaa jirani yake wakati wakijisomea masomo ya usiku (Prepo) alikuwa akimsikia.
“Unataka kuona? Jafet, nimekusikia vizuri au naota?”“Aaah...eeh aah....eee,” Jafet alibabaika huku akijisikia aibu kubwa kwani hakutegemea kama rafiki yake huyo anaweza kumsikia.
“Sheria za upadri haziruhusu kuwa na mke wala kuwa na mtoto, isitoshe ni dhambi kubwa kwa Mungu kufanya mambo hayo kama umeshaamua kumtumikia kupitia upadri,” Gervas, rafiki yake Jafet aliyekuwa akisoma naye, alianza kumpa somo.
Japokuwa Jafet alikuwa anaijua sheria hiyo, siku zote ndani ya moyo wake alikuwa akitamani akiwa mkubwa, aje kuw ana familia na tayari akili zake zote zilishahamia kwa Anna, akashusha pumzi ndefu wakati Gervas akiendelea kumuelimisha juu ya madhara ya kufanya vile alivyokuwa anafikiria.
“Tena uongozi wa shule ukishakugundua mapema kwamba huna nia ya dhati ya kuja kuwa padri, huo ndiyo utakuwa mwisho wako hapa shuoleni, utafuikuzwa na hutapata tena nafasi ya kurudi,” alisema Gervas, kauli iliyokuwa kama mkuki ndani ya moyo wa Jafet.
Alikumbuka jinsi alivyokuwa analia kwa uchungu baada ya kufaulu lakini wazazi wake wakashindwa kumuendeleza kutokana na ufukara wa hali ya juu uliokuwa ukiikabili familia yake. Alikumbuka jinsi alivyopata bahati ya mtende kuota jangwani baada ya mama yake kusikia habari za mapadri na hatimaye kumuunganisha naye.
Alikumbuka jinsi alivyofurahi siku ya kwanza alipowasili shuleni hapo na kuyaanza rasmi masomo ya sekondari, akigharamiwa kila kitu na mapadri, akajikuta nafsi yake ikimsuta kwamba alichokuwa anakifanya hakikuwa sahihi.
“Lakini nampenda sana Anna!” alisema huku uso wake ukionesha kuanza kujawa na huzuni kubwa.
“Uamuzi ni wako, unaweza kuchagua kati ya Anna na maisha yako, ila mi nimekupa tu angalizo,” alisema Gervas huku akikusanya vitabu vyake na kuondoka kurudi bwenini, akamuacha Jafet akiwa amezama kwenye dimbwi la mawazo, akiwa hajui nini cha kufanya

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

NINI MAANA YA MAPENZI

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU