JE WATAKA KUJUA NAMI NAKUJUZA NANI NI NANI URAISI PROFESA IBRAHIM LIPUMBA
Kwa ufupi
Alipata elimu ya msingi mkoani Tabora mwaka 1959
katika Shule ya Wamisionari wa Sweden waliokuwa Tanzania wakati huo,
shule hiyo iliitwa “Swedish Free Mission Primary School”, alimaliza
mwaka 1962 na akasoma Shule ya Kati (Middle School) mwaka 1962 – 1966
kabla ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari
Tabora mwaka 1967 – 1972 kisha akaelekea mkoani Dar es Salaam na kusoma
kidato cha tano na sita katika Shule Sekondari ya Pugu kati ya mwaka
1971-1972...
Historia yake
Ibrahim Lipumba ni mchumi wa kimataifa na
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF). Alizaliwa Juni 6, 1952 katika
Kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora.
Alipata elimu ya msingi mkoani Tabora mwaka 1959
katika Shule ya Wamisionari wa Sweden waliokuwa Tanzania wakati huo,
shule hiyo iliitwa “Swedish Free Mission Primary School”, alimaliza
mwaka 1962 na akasoma Shule ya Kati (Middle School) mwaka 1962 – 1966
kabla ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari
Tabora mwaka 1967 – 1972 kisha akaelekea mkoani Dar es Salaam na kusoma
kidato cha tano na sita katika Shule Sekondari ya Pugu kati ya mwaka
1971-1972.
Alipata shahada mbili za kwanza katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) na mbili nyingine amezipata katika Chuo Kikuu
cha Stanford, Marekani ambacho ni miongoni mwa vyuo 10 bora duniani.
Shahada zote nne alizonazo ni za uchumi.
Alisoma na kupata shahada ya kwanza katika uchumi mwaka 1973 - 1976 na shahada ya Uzamili akiianza mwaka 1976 - 1978. Lipumba ni miongoni mwa
Watanzania waliowahi kuweka rekodi nzito UDSM katika shahada ya kwanza,
ndiye aliyekuwa mwanafunzi bora katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya
Jamii akiwa amepata daraja la kwanza la juu kuliko wanafunzi wote (GPA
5) na alitunukiwa zawadi ya Makamu Mkuu wa Chuo katika Kitivo cha Sanaa
na Sayansi ya Jamii.
Profesa Lipumba alipojiunga Chuo Kikuu cha
Stanford alisoma shahada mbili na kupata ufaulu wa heshima, kwanza
alisoma na kuhitimu Shahada ya Uzamili mwaka 1977/1978 na kisha akasoma
na kuhitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika uchumi kati ya mwaka 1978 –
1983. Kwa ujumla, elimu ya uchumi ya Profesa Lipumba imejikita katika
masuala ya fedha na biashara za kimataifa na eneo la pili ni maendeleo
ya uchumi na uchumi wa kilimo.
Kwa miaka mingi sasa Profesa Lipumba amekuwa
mhimili mkubwa wa masuala mbalimbali ya uchumi duniani, ameshiriki
katika majopo ya wanazuoni nguli wa uchumi duniani katika kutafuta mbinu
bora za kusaidia nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kujikwamua
kiuchumi. Ameshiriki moja kwa moja katika shughuli za kitaalamu
kutathmini uchumi wa nchi nyingi duniani na kutoa mapendekezo ya hatua
za kuchukua, amefundisha katika vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani na
amewatumikia Watanzania katika nyanja za kiuchumi kwenye Serikali
kadhaa.
Alianza ajira akiwa mhadhiri msaidizi UDSM na
akawa mhadhiri mwandamizi baada ya kuhitimu PhD, alikuwa profesa
mshiriki kuanzia mwaka 1989 kabla ya kuwa profesa miaka ya 1990.
Kimataifa amekuwa profesa mwalikwa katika Kituo cha Maendeleo ya
Uchumi katika Chuo cha Williams Marekani 1989 – 1993, mtafiti
mwandamizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uchumi
(UNU/WIDER) kilichopo Finland mwaka 1993 – 1995.
Amekuwa akisimamia masuala ya uchumi wa dunia kwa
ngazi ya ushauri wa kimataifa, amekuwa mchumi mshauri wa Umoja wa
Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF), UNDP, Sida,
Norad, Danida, mashirika ya kikanda kama Comesa na baadhi ya nchi za
Afrika, Ulaya na Asia.
Amefanya kazi kubwa za kiushauri ili kuinua
mashirika mbalimbali ya umma nchini, amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya
TKAI, NIC, TWICO, Imara Wood Industries, Tume ya Rais ya kushughulikia
masuala ya uchumi wakati wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi,
mwenyekiti wa tume kadhaa zilizoundwa na Rais za uchunguzi wa matatizo
ya mashirika mbalimbali ya umma.
Profesa Lipumba amezaliwa na kukulia katika
familia ya kisiasa. Baba yake mzazi ni miongoni mwa waasisi wa Tanu na
alishiriki mkutano wa mwaka 1958 uliojadili kuharakishwa kwa uhuru wa
Tanganyika. Mwenyewe amekuwa kada wa Tanu na baadaye CCM tangu akisoma
hadi alipokuwa anafanya kazi.
Mbio za ubunge
Profesa Lipumba hajawahi kugombea ubunge tangu alipojiunga na siasa.
Mbio za urais
Miaka michache baada ya vyama vingi kuanzishwa alijiunga na CUF.
Moja ya mambo yaliyomsukuma ni kule kuona mambo mengi ambayo yeye na
wenzake walikuwa wakiishauri Serikali ili kuinua uchumi wa nchi yalikuwa
hayafanyiwi kazi au yanafanyiwa kazi kisiasa na matokeo yake uchumi
unazidi kudidimia na umaskini unaongezeka. Profesa Lipumba ameoa na ana
watoto wawili.
Mbio za ubunge
Profesa Lipumba hajawahi kugombea ubunge tangu alipojiunga na siasa.
Mbio za urais
Profesa Lipumba alianza mbio za urais mwaka 1995
kupitia CUF akaibuka nafasi ya tatu kwa asilimia 6.43, akiwa nyuma ya
mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa (asilimia 61.82) na Augustine Mrema wa
NCCR (asilimia 27.77).
Mwaka 2000, aligombea urais kwa mara ya pili na
kushika nafasi ya pili akipata asilimia 16.26 ya kura zote. Huu ni
uchaguzi ambao Rais Mkapa wa CCM aliibuka mshindi kwa kupata asilimia
71.74 ya kura zilizopigwa.
Mwaka 2005, CUF ilimpa tena kazi hiyo kwa mara ya tatu,
alipambana vilivyo na mwanasiasa maarufu wakati huo, Jakaya Kikwete wa
CCM na kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68. Kikwete alikuwa
na asilimia 80.28.
Mwaka 2010, CUF ilimtaka akatupe karata kwa mara
ya nne, safari hii aliibuka mshindi wa tatu kwa kupata asilimia 8.28
nyuma ya Rais Kikwete wa CCM aliyekuwa na asilimia 62.83 na Dk Willibrod
Slaa wa Chadema aliyepata asilimia 27.05.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Profesa Lipumba
ni mmoja wa Watanzania mashuhuri wanaotajwa kuwa na sifa, uwezo, vigezo
na nafasi ya kuwa Rais wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya
upinzani vyenye wabunge nchini vimeweka azimio la kusimamisha mgombea
urais mmoja kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mwezi uliopita akiwa mkoani Tabora alitangaza
kwamba atachukua fomu na kukiomba chama chake kimpe fursa ya kufanyiwa
tathmini na wagombea wengine wa Ukawa ili kumpata mtu mmoja
atakayesimama katika nafasi hiyo.
Nguvu yake
Sifa na nguvu yake ya kwanza ni umaarufu na
kuheshimika ndani na nje ya nchi. Hakuna mahali popote katika nchi hii
utakapotaja jina lake watu wasimfahamu, lakini hata kimataifa
wanamfahamu vizuri kwa uchapakazi wake na misimamo yake katika ukuzaji
wa uchumi. Kinachonistaajabisha ni kuwa, si mtu wa kupenda kutumia
umaarufu wake kufanya “siasa rahisi” (cheap politics). Anaamini kuwa
siasa si ujanjaujanja wala jambo la masihara.
Lakini jambo la pili ni uadilifu na uwazi. Kwa bahati nzuri
nimefanya kazi naye kwa zaidi ya miaka mitano na namfahamu katika eneo
hili. Hata mara moja ndani ya chama chake hawezi kujaribu kuingilia
masuala ya fedha na hayamhusu kabisa lakini pia anachukia mbinu zozote
zile ambazo zinaweza kufanywa ndani ya chama chake na hata nje, ambazo
zitaleta taswira ya kukosa uaminifu kwenye fedha.
Nadhani ndiyo sababu kuu kwamba CUF kwa muda mrefu
imekuwa ikipata madhara kidogo katika ukaguzi wa hesabu zake za fedha,
kulinganisha na vyama vingine vyote vinavyopokea ruzuku kutoka
serikalini na hata michango ya wanachama.
Tatu, Profesa Lipumba ni mtu wa kawaida na anaishi
maisha ya kawaida. Hupenda kufanya mazoezi mara kwa mara na haiwezekani
apite bila kukusalimia. Nakumbuka mwaka 1995 alipoanza kampeni za urais
alikuwa anatumia “kigari” cha milango miwili tu, wa dereva na wa kwake,
alikitumia kuzunguka nchi nzima bila kuhofia kuwa hadhi yake si ya
kuendeshwa na kigari kama kile. Ni wanasiasa wachache Afrika wenye
ustahimilivu na maisha haya.
Ni Mtu wa kujitolea. Nimeshuhudia CUF ikimlipa
kiongozi huyu shilingi milioni moja tu kwa mwezi za posho (CUF hawalipi
mishahara). Kwa mwaka, anaweza kutumia posho yake ya miezi hadi sita
akielekeza (posho nzima) ipelekwe mahali fulani kusaidia wagonjwa au
watu wengine. Kuna wakati amewahi kuniagiza (nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa
CUF), kupeleka posho yake yote ya mwezi kwa waathirika wa mabomu ya
Arusha. Haishi kwa kutegemea siasa, anaamini siasa si ajira wala sehemu
ya kujinufaisha na ndiyo maana hata mimi hadi leo hii nimekuwa na
mtazamo na msimamo wa namna hiyo.
Mwisho, huenda ndiye mwanasiasa pekee (kwa siasa
za kuanzia mwaka 1995 – 2015) aliyewahi kuzunguka Tanzania na kushuhudia
matatizo ya wananchi kuliko mtu mwingine yeyote. Kila mwaka anatumia
wastani wa siku hadi 130 akiwa kwenye ziara za ujenzi wa chama mikoani
lakini kila baada ya miaka mitano kuanzia mwaka 1995 alipata wasaa wa
kuzunguka, bila kupumzika, kwenye majimbo yote kuomba kura kwa wananchi.
Sijui nani mwingine ameweka rekodi hii.
Udhaifu wake
Kwa siasa za Tanzania, moja ya udhaifu mkubwa wa
Profesa Lipumba ni kuchukulia kila jambo kitaaluma, “He is too
academic”. Hali hii inamfanya wakati mwingine asieleweke kwa watu
wanaomsikiliza. Mathalan, anaweza kuhutubia wananchi na akatumia muda
mwingi kutoa takwimu za Benki ya Dunia au masuala ya tafiti za
kutaalamu. Watanzania wengi hawana elimu kubwa na hata waliosoma wana
ufahamu wa kadri mno, kuwapangia mikakati ya uhuishaji wa siasa na nchi
kitaaluma kunawafanya wasijue mipango inayoongelewa.
Kuna wakati huzungumzia masuala ya uchumi na
maendeleo na akamaliza mkutano na waandishi wa habari, akishaondoka
waandishi wanakufuata na kukuuliza mambo mengi yanayohitaji ufafanuzi.
Akiwa mtu ambaye anatajwa kuwa na sifa na vigezo vya urais, udhaifu huu
unamfanya asifikishe ujumbe wake wa mabadiliko kirahisi.
Pili, ni mtu aliyeweka familia yake mbali na
siasa, Hili si jambo dogo. Kuna watu hawakumpigia kura katika chaguzi
alizoshiriki kwa kupewa propaganda kali kuwa hana mke na hajawahi kuwa
na mke wala mtoto. Ukweli ni kuwa Lipumba ana mke na watoto wawili
wakubwa, ni mmoja wa wanasiasa wenye familia na ndoa imara huku akijua
majukumu yake ya ulezi wa familia katika jamii. Sielewi kwa nini hapendi
kuchanganya familia yake na siasa kwa sababu taswira anayoipata kwa
jamii kutokana na uamuzi huo nadhani siyo nzuri. Ndiyo maana wengi
wanadhani yeye ni “Senior Bachelor”.
Mwisho, kuna nyakati hatumii nafasi yake ya
uenyekiti wa chama sawasawa. Ameacha mambo mengi yaamuliwe kwa mawazo,
maoni na ushauri wa watu waliomzunguka kuliko kufanya uamuzi mgumu
wakati mwingine akiwa mwenyekiti. Anataka kila jambo liamuliwe kwa
pamoja na sikuwahi kuona hata mara moja akiamua jambo peke yake, sielewi
kama ni lengo la kukwepa lawama za uamuzi au ni utaratibu wake. Kwa
siasa za Afrika, kiongozi wa juu wa taasisi kuna nyakati nyingi tu
anapaswa achukue uamuzi mwenyewe na abebe lawama mwenyewe kwani huwezi
kuwa na uhakika kama watu wote waliokuzunguka wana uwezo wa kukushauri
vizuri muda wote.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo kadhaa yanaweza kufanya CUF impitishe kugombea urais na kurahisisha pia tiketi yake ndani ya Ukawa:
Moja, msomi mahiri wa uchumi katika ngazi ya kimataifa na kwa
Tanzania, amekuwa akionekana kama mchumi bora zaidi kuliko wote. Profesa
Kitila Mkumbo, Mhadhiri wa UDSM katika andiko lake juu ya kiongozi
huyu, anaeleza kuwa “…Wasomi kadhaa wa uchumi niliozungumza nao
wanaamini kwamba Profesa Lipumba ndiye mchumi bora zaidi hapa Tanzania.
Aidha, pamoja na kwamba yupo katika siasa, Profesa Lipumba ameendelea
kuheshimika katika taaluma ya uchumi duniani. Hata hivyo, taaluma yake
imekuwa haitumiki ipasavyo hapa nyumbani kwa sababu watawala wetu hujali
ufuasi wa vyama zaidi kuliko utaalamu wa mtu katika kupanga watu katika
nafasi nyeti za kazi”. CUF na Ukawa nadhani vinahitaji mgombea mwenye
sifa hii.
Pili, naamini kwa siasa za upinzani za Tanzania,
Profesa Lipumba ndiye kiongozi pekee mwenye uzoefu mkubwa wa kusimamia
masuala ya kimataifa kumshinda mtu mwingine yeyote. Ametumia sehemu
kubwa ya maisha yake akisimamia miradi mikubwa ya kiuchumi katika nchi
nyingi na mashirika ya kimataifa duniani. Uzoefu wa kimataifa ni turufu
muhimu kwa kiongozi yeyote wa kisiasa.
Mwisho, ana uzoefu mkubwa na utendaji wa ngazi ya
juu ndani ya Serikali kwa sababu amefanya kazi serikalini, ameshauri
mambo mengi kuhusu uhuishaji wa mashirika ya umma, amekuwa mtu muhimu
kiushauri kwenye miaka ya nyuma katika Benki Kuu ya Tanzania na
nyinginezo. Rekodi hizi nadhani zinakifanya chama chake kimpe nafasi
kubwa kabisa kumshinda mtu yeyote yule na huenda hata ndani ya Ukawa
awaka na sifa za juu kuwashinda wanasiasa wengine.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo moja tu ndilo naliona kama kikwazo kwake.
Ikiwa makubaliano ya ndani ya Ukawa yataonyesha kuwa CUF haipaswi kutoa
mgombea urais kwa sababu labda umoja huo umeamua mgombea atoke kati ya
NCCR, NLD na Chadema. Hili peke yake ndilo linaweza kumkwamisha.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Kwa mtizamo wangu, ikiwa hatagombea urais mwaka
huu na labda kutochaguliwa na chama chake, Ukawa inaweza kumtumia
kugombea ubunge kwenye majimbo ya Kinondoni, Segerea au Temeke. Watu
wengi niliozungumza nao wanaumia kwa kumkosa bungeni.
Mfano wa umuhimu wake kwenye vyombo vya uamuzi wa
mambo makubwa ya nchi ulijidhihirisha kwenye Bunge la Katiba. Nitaumia
hatagombea urais halafu tena asigombee ubunge. Pia, ikiwa Ukawa
itashinda uchaguzi wa mwaka huu, simuoni waziri mkuu bora wa Serikali ya
kisasa kama Profesa Lipumba.
Lakini pia kama hatagombea urais nadhani atakuwa
na jukumu la kuongoza chama chake kwa miaka minne ya kipindi chake
ambacho nadhani ni cha mwisho kabisa, kuendelea kuishauri Serikali ijayo
bila kujali itaundwa na Ukawa au CCM na kuendelea kufanya kazi za
kitaalamu za kitaifa na kimataifa.
Hitimisho
Sikupata shida kumtathmini Profesa Lipumba kwa
sababu nimefanya naye kazi kwa karibu. Watu waliofanya kazi chini yake
wamejifunza bidii kazini, nidhamu, kutunza muda, kuchukulia siasa kama
kazi ya kujitolea na kusaidia wananchi na kuamini kuwa siasa inawajibika
kutumikia uchumi. Ni mmoja wa wanasiasa wa kweli na wanaochukia
mikakati ya ki-propaganda hata kutoka ndani ya chama chake. Sielewi ni
wanasiasa wangapi nchi hii wana uwezo, uthubutu, elimu, umashuhuri,
wajibikaji na kujituma kama kiongozi huyu. Namtakia kila lililo jema
katika safari yake ndefu katika siasa za Tanzania.
Comments
Post a Comment