BALOZI AJIPANGA KUTOKOMEZA MAUAJI YA ALBINO
Henry
Mdimu (katikati anayezungumza) akitoa ufafanuzi wa namna ya kutoa elimu
juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi 'Albino' huku kushoto
akiwa ni Mratibu wa Fedha na Udhamini wa Imetosha, Monica Joseph na
Masoud Kipanya ambaye naye ni mmoja wa wakilishi wa Imetosha
.
Mwakilishi
wa Tanzania Bloggers Network, Joakhim Mushi (kushoto) akielezea namna
ya kuweza kusambaza taarifa ya kupinga ukatili dhidi ya mauaji ya Albino
kupitia vyombo vya habari.
BALOZI wa kujitolea wa harakati za imetosha, Henry
Mdimu amezungumza na wanahabari juu ya kukomesha mauaji dhidi ya watu
wenye ulemavu wa ngozi, maarufu Albino unaoendelea hivi sasa .Akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar, Mdimu alisema kuwa dhumuni lake kuu ni kutaka kueleza ulimwengu kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya harakati ya ‘Imetosha’ambayo ameianzisha yeye.
Alisema, ameamua kuanzisha ishu hiyo baada ya kushuhudia ndugu zake wenye ulemavu wa ngozi wakiteseka kwa muda mrefu huku akiongeza kuwa alishindwa kuanzisha harakati hizo kwa kuviamini vyombo vinavyohusika na utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Hata hivyo, alisema ameamua kuweka jitihada zake binafsi ili kuisaidia serikali kuondoa doa linaloichafua nchi hii yenye amani, hivyo amewaomba Watanzania wote kushikamana kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alitoa ufafanuzi kwa kumnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akisema kuwa kati ya mwaka 2006 hadi 2015, watuhumiwa 139 wameshikiliwa ambapo kesi 35 zimeandikishwa huku watuhumiwa 73 wakiachiwa huru na wengine 15 wamekamatwa na makosa hayo.
“Kutokana na ushawishi nilionao kama mwandishi na mtangazji wa redio pia ni Blogger, ninaamini nitaleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha haki ya kuishi kwa ndugu zangu inaheshimiwa na kubaki kama walivyo watu wengine.
“Nina mpango wa kwenda Kanda ya Ziwa kuhangaika na hili mpaka nione mwisho wake kwani tatizo ni rahisi kulimaliza kabla halijaenea nchi nzima maana walemavu wapo nchi nzima lakini kabla ya hapo Machi 21, mwaka huu kutakuwa na matembezi ya hisani ya kilomita tano hapa jijini Dar ya kupinga ukatili huo ambayo yataanzia katika viwanja vya Leaders kupitia Kinondoni Manyanya na kurudi viwanjani hapo .
“Mimi pamoja na wanaharakati wenzangu tutaondoka kuelekea Mwanza kwa ajili ya kutoa elimu kwa njia ya sanaa tukiwa na washauri nasaha pamoja na wasanii wa muziki wanaoandaa nyimbo mabalimbali zenye ujumbe wa kutokomeza ukatili huu,” alisema Mdimu.
Comments
Post a Comment