JE WAJUA MBEGU MABOGA ZINA UWEZO WA KUKUEPUSHA NA MAGONJWA MBALIMBALI....


http://samwelmlawa.blogspot.com
                                                     Mbegu za maboga
Na.samwelmlawa
ZIKIWA zimesheheni protini na madini kadhaa kama vile chuma, kopa, maginizia, manganizi na zinki, mbegu za maboga zinakuwa mbegu bora na muhimu kutafuna kila wakati kama wewe ni mpenzi wa kutafuna-tafuna. Imethibitika pasipo na shaka kuwa mbegu za maboga zina faida lukuki kiafya na zina uwezo wa kukuepusha na magonjwa hatari zaidi ya 10:

UGONJWA WA MOYO
Mbegu za maboga zina kiasi kingi cha madini aina ya maginizia (magnesium) ambayo huboresha utendaji kazi wa viungo vya mwili. Huimarisha  usukumaji wa damu kwenye moyo, huimarisha ukuaji wa mifupa na meno, huifanya mishipa ya damu kupitisha damu kwa urahisi na hufanya upatikanaji wa haja kubwa kuwa laini.
KINGA YA MWILI
Mbegu za maboga pia zina kiasi kingi cha madini ya Zinki (Zinc). Madini haya yana faida nyingi mwilini, ikiwemo kuimarisha kinga ya mwili, kuboresha ukuaji na uundaji wa chembechembe hai za mwili, kuboresha usingizi, kuboresha ladha mdomoni na harufu, huboresha afya ya macho na ngozi, hurekebisha sukari na huboresha nguvu za kiume pia.
Upungufu wa madini ya ‘Zinc’ mwilini una uhusiano mkubwa sana na matatizo ya kuzaa watoto njiti, kuota chunusi nyingi mwilini, watoto kuwa na uwezo mdogo darasani kimasomo na matatizo mengine mengi ya kimwili na kiakili.
MAFUTA YA OMEGA -3
Omega-3 ni moja kati ya mafuta muhimu sana mwilini. Jamii ya karanga pamoja na mbegu za maboga ni miongoni mwa mbegu zenye kiasi kingi cha mafuta aina hii. Hivyo ulaji wa mbegu za maboga utakuwezesha kupata kirutubisho hiki muhimu katika mwili wako na kukupa faida za mafuta haya ambazo ni nyingi.
KIBOFU CHA MKOJO
Tangu enzi za mababu zetu, mbegu za maboga zimetumika kuimarisha afya ya wanaume kutokana na kuwa na kiasi kingi sana cha madini aina ya Zinc ambayo ni muhimu sana kwa afya ya kibofu cha mkojo. Mbegu za maboga pamoja na mafuta yake, yote kwa pamoja hutoa kinga kwenye kibofu kupatwa na matatizo ya kiafya, yakiwemo yale ya saratani ya kibofu.
KINGA DHIDI YA SARATANI
Imethibitika kwamba watu ambao hula mlo wenye kiasi kingi cha mbegu za maboga wamegundulika kuwa na hatari ndogo sana ya kupatwa na saratani za tumbo, matiti, mapafu na kibofu.

UGONJWA WA KISUKARI
Utafiti uliofanywa kwa kuwalisha wanyama mbegu za maboga, umeonesha kuwa ulaji wa mbegu za maboga, husaidia kurekebisha kiwango cha ‘Insulin’ mwilini na hivyo kumuepusha mtu kupatwa na ugonjwa wa kisukari.
MATATIZO YA UKOMO WA HEDHI
Mara nyingi kina mama watu wazima ambao wamefikia ukomo wa hedhi, hupatwa na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na hali hiyo. Hata hivyo utafiti umeonesha kuwa mbegu za maboga zina uwezo wa kurekebisha hali hiyo na kuondoa kabisa matatizo ya kiafya yatokanayo na ukomo wa hedhi.
AFYA YA MOYO NA MAINI
Mbegu za maboga, ambazo zina kiasi kingi cha mafuta mazuri, kamba lishe na virutubisho vinavyoimarisha kinga ya mwili (antioxidants), zimeonekana kuwa bora pia kwa afya ya moyo na ini, huweza kumpatia mlaji kinga dhidi ya matatizo ya kiafya katika moyo na ini.
DAWA YA USINGIZI
Mbegu za maboga zimegundulika pia kuwa na kirutubisho kinachozalisha ‘homoni’ za usingizi. Ulaji wa mbegu za maboga saa chache kabla ya kupanda kitandani, hasa ukila pamoja na tunda lolote, kunasaidia kupata usingizi mzuri na tulivu.
DAWA YA UVIMBE
Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa mbegu za maboga zina mafuta yenye uwezo wa kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya uvimbe (inflamatory diseases) sawa na dawa aina ya ‘indomethacin’, lakini mbegu hizi hazina madhara kama ilivyo kwa hiyo dawa.
JINSI YA KULA MBEGU ZA MABOGA
Ili kupata faida zake zote, zikiwemo zile za mafuta yake, inashauriwa kula mbegu hizo zikiwa kavu, bila kuzikaanga. Hakikisha pia unapata mbegu zilizohifadhiwa vizuri ambazo hazijaoza wala kuwa na fangasi. Iwapo utapenda kuzikaanga, basi hakikisha unazikaanga kwa muda usiozidi dakika 15, unaweza pia kuongeza chumvi kidogo kupata ladha, lakini za kukaanga zitakuwa hazina mafuta mengi kama zile kavu.
           kwa mawasiliano zaidi
              samwelmlawa@ymail.com
              Iskakanews@gmail.com
                                            karibu.......

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

NINI MAANA YA MAPENZI