DIAMOND, WEMA WATANGAZA NDOA

Stori: Shakoor Jongo na Imelda Mtema
HUKU mchumba’ke, Penniel Mungilwa ‘Penny’ akifungasha virago kurejea kwao, mzee mzima Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ametangaza kumuoa Miss Tanzania 2006, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’.
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’(kushoto) na Penniel Mungilwa ‘Penny’ wakiongea jambo enzi za mapenzi yao.
Ishu hiyo ilijiri ndani ya Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar ambapo mkali huyo wa Bongo Fleva alikuwa akikamua kwenye sherehe ya Krismasi aliyoiandaa mwenyewe.

Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya kupanda jukwaani katika viwanja vya leaders.
TANGAZO LA AWALI
Awali kabla ya kufikia eneo la kutangaza kuoana, Diamond aliweka wazi jukwaani kwamba yeye na Wema wamerudiana.
Diamond Platnumz akiongea jambo baada ya Wema Isaac Sepetu ‘Madam’  kupanda jukwaani.
MTIRIRIKO ULIVYOKUWA
Diamond, akiwa ameshika kipaza sauti alikatisha kuimba na kuwauliza mashabiki wake, hasa watoto waliohudhuria kwa wingi tamasha hilo, je, wanataka kumuona shemeji yao?
“Itakuwa si vizuri mkaondoka bila kumuona shemeji yenu, nikuleteeni mumuone?” aliuliza  Diamond. Swali hilohilo akalirudia tena ambapo lilipokelewa kwa shangwe huku mashabiki wakilitaja jina la Wema.
                                        Diamond Platnumz na Wema Isaac Sepetu wakijiachia.
WEMA APANDISHWA JUKWAANI
Kufuatia kelele za mashabiki, Diamond alimuomba Disco Joker (DJ) wake amuwekee Wimbo wa Ukimwona ambao ulisindikiza ujio wa Wema jukwaani akifuatana na wapambe wa Diamond.
“DJ acha huo, nipigie Wimbo wa Ukimwona watu wangu wa nguvu wamwone shemeji yao kwani tangu nilivyokwenda naye China walikuwa wakisumbuliwa na maneno tofautitofauti kutoka kwenye mitandao ya kijamii,” alisikika Diamond.
Diamond, akiwa ameshika kipaza sauti akiima Wimbo wa Ukimwona na Wema akiwa amemkumatia.
JUKWAA SASA
Hali haikuwa ya kawaida jukwaani kwani kilichofuata hapo ni Wema kuonesha kwa vitendo mambo yaliyoashiria kuwa, wawili hao sasa ni mwendo mdundo.
Wema alishuhudiwa akimzungushia mikono Diamond kwenye kiuno jambo ambalo liliwafanya baadhi ya mashabiki wa mastaa hao kutoa machozi ya furaha kuona penzi la wawili hao limerudi upya, wengine walimwambia Diamond amuoe Wema.
“Diamond muoe Wema, mnapendezana sana,” walisikika mashabiki.
Wema Isaac Sepetu ‘Madam’akimuaga Diamond Platnumz kwa kumkumatia.
MAWIFI WADAI KUHARIBIWA SIKU NA KAKA YAO
Hata hivyo, kitendo cha Diamond kumwita Wema jukwaani kilionekana kuharibu furaha ya sikukuu kwa ndugu zake kwani bila ya kuuma midomo dada zake staa huyo wakiongozwa na Esma Khan walinuna na kuanza kuondoka.
“Yaani siku yangu imeshaharibika, nilikuja nina furaha sasa imepotea, tuondokeni ndugu zanguni,” alisema Esma akiwaambia Mwanaisha Abdul ‘Queen Darleen’ na Halima Haroun ‘Kimwana’.

Diamond Platnumz na Penny wakiwa pamoja enzi za mapenzi yao.
MAMA DIAMOND ASHANGAA
Kitendo cha ndugu hao kukasirika hakikupokelewa vizuri na bi mkubwa wao yaani mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ ambaye aliwajia juu akiwashangaa.
“Wajinga nini? Sasa walitaka Diamond… (tusi) wao, mtu ameshaamua kupenda wamwache, mi’ mwenyewe nimeshajifunza, sitaki kuingilia penzi lake,” alisema mwanamke huyo ambaye mjini anazungukia usafiri aina ya Altezza.
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’  na Penniel Mungilwa ‘Penny’.
Baada ya shoo hiyo iliyomalizika saa moja usiku, paparazi wetu alimfuata Diamond akiwa amesimama na Wema na kuwauliza kama kweli wana nia ya kufunga ndoa.
“Hilo mwana mbona lipo wazi, nataka kumuoa staa na nataka kuzaa na staa,” alisema Diamond huku Wema akiwa hapingi.

MAMA WEMA ATANGAZA VITA  NA DIAMOND
Wakati Dimaond akitambia ndoa na Wema, siku hiyohiyo ya Krismasi, mama wa Wema, Mariam Sepetu alidaiwa kutangaza vita na mwanamuziki huyo baada ya kusikia tetesi kuwa amerudiana na mwanaye.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa mama Wema (jina tunalo) mama wa staa huyo alichukizwa na kitendo cha Diamond kurudiana na mwanaye kwani anaamini anamchezea tu.
Mama wa Wema, Mariam Sepetu.
Rafiki huyo alizidi kudai kuwa, taarifa hizo zimemuweka  mama huyo kwenye wakati mgumu na kudai kuwa popote atakapokutana na mwanamziki huyo atampopoa mawe au machungwa hata ikiwa siku ya ndoa yao.
“Mama Wema amesema hampendi Diamond, popote atakapomuona itakuwa vita ya wawili, kama kuna jiwe atamrushia, hata machungwa kama yapo yatakuwa halali yake,” alisema rafiki huyo.

WOSIA WA MZEE SEPETU
Mpashaji huyo wetu alizidi kufunguka kuwa, mama Wema ana wosia mkononi ambao aliuacha marehemu mumewe, mzee Isaac Abraham Sepetu.
Alisema katika wosia huo, mzee huyo alisema hataki Diamond amuoe Wema na kama mrembo huyo atakiuka  wosia huo atapatwa na laana mbaya katika maisha yake.
“Kinachomuumiza zaidi mama Wema ni huo wosia, mzee Sepetu alisema hataki mtoto wake aolewe na Diamond, kama atakataa kuna kitu kibaya kitamkuta katika maisha yake,” alisema rafiki huyo.

MAMA WEMA ASAKWA
Baada ya kupata habari hizo, gazeti hili lilimvutia waya mama Wema ili kuweza kuthibitisha madai hayo ambapo alisema kuwa, hayuko tayari kuzungumzia jambo hilo kwa wakati huo mpaka atapoamua akisisitiza muda si mrefu.
“Jamani nina mambo mengi sana ya kufanya na sijatulia kabisa siko tayari kuzungumza chochote kwa sasa nikiwa tayari nitawaambia kila kitu,” alisema mama Wema.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

NINI MAANA YA MAPENZI

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU