Rage arudishwa madarakani


Ismail Aden Rage.

BARAZA la Wadhamini la Klabu ya Simba, limesikia maamuzi yaliyofanywa na kikao cha kamati ya utendaji ya timu hiyo, juu ya kumsimamisha mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage na kusema lenyewe bado linamtambua kiongozi huyo.

Hamis Kilomoni, ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, maamuzi ya kamati ya utendaji ya timu hiyo hayakufuata katiba kikamilifu, hivyo baraza lake linaendelea kumtambua Rage kama mwenyekiti halali wa Simba.
Kilomoni, ambaye ni nyota wa zamani wa timu hiyo, amesema juzi aliitisha kikao cha baraza lake na kukutana na mwenzake Ramesh Patel, ambapo wamegundua kwamba kamati  haikufuata katiba kikamilifu.
Alisema kamati hiyo ya utendaji ilitakiwa kuyachukua maamuzi yake na kuyawasilisha katika baraza la wadhamini au lile la wazee, ambayo yote yanaongozwa na yeye.
Hata hivyo, Kilomoni alibabaika wakati akitoa maelezo yake baada ya kuulizwa inakuwaje wadhamini ambao kazi yao ni kuangalia mali za klabu, waingilie uamuzi wa kiutendaji!
“Kweli hatujaingilia, lakini tunachotaka ni kuwakutanisha baada ya Rage kutua kesho (leo) usiku,” alisema na alipoulizwa inakuwaje wametengua uamuzi wa kamati ya utendaji na kuendelea kumtambua Rage, alisema:
“Sasa sijui unavyofikiri ila sisi tunataka kulimaliza hili suala, unajua tumekutana mimi na Ramesh Patel ambao ndiyo wadhamini, mmoja wetu anaishi Uarabuni na tusingeweza kushirikisha baraza la wazee kwa kuwa halipo.
“Maamuzi waliyoyafanya vijana wetu tunayaona kama yana kasoro, katiba haiwaruhusu kuchukua maamuzi ya aina hiyo, ni kama wamefanya maamuzi kwa jazba kubwa, jambo ambalo tunaona siyo sahihi.”
Kilomoni alipoulizwa ni kipengele kipi cha katiba kinawaruhusu kutotambua maamuzi ya kamati ya utendaji, alijiuma:
“Aah mi sikijui, labda nirudi na kufungua katiba nitafute tena lakini kikubwa tunataka kusuluhisha.”
Kuhusiana na kurejea kwa Rage, Kilomoni alisema hatambui kama atarejea na matarumbeta na kupokewa na wanachama.
“Sijui lolote, hajaniambia kama anataka kufanya hivyo. Lakini pia sijui lolote kuhusiana na mkutano wa Jumapili ambao Rage inasemekana atauitisha, nimesikia tu lakini sijui,” alisema.
Awali, ilielezwa kuwa, baada ya Rage kurejea na kupokewa kwa mbwembwe, atafanya mkutano keshokutwa Jumapili na kuwatimua wajumbe wote wa kamati ya utendaji ambao walimsimamisha na kuitisha mkutano Desemba Mosi ambao utatoa uamuzi wa mwisho arudi madarakani au ndiyo ‘apigwe chini kimoja’.
Awali, katika hali iliyoonekana ni ya kushangaza, Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’, alikuwa amepanga kuzungumza katika mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo, Msimbazi, Kariakoo jijini Dar, lakini akaukimbia, ndipo waandishi walipoelezwa waende Kinondoni kwa mzee Kilomoni kwa ajili ya mkutano huo.
Kuhusiana na mgogoro huo wa Simba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema limepokea barua kuhusiana na kusimamishwa kwa Rage na nafasi yake kuchukuliwa na Mzee Kinesi.
“Tumepokea barua na sasa tunasubiri suala hilo tutalipeleka kwenye kamati ya sheria,” alisema Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura.
Hata hivyo, hakuna kamati yoyote hadi sasa tangu uongozi mpya uingie madarakani chini ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi ambaye juzi alisema watakutana kesho na kuziunda upya.
Siku moja baada ya kusimamishwa na kamati ya utendaji kwa madai ya ubadhirifu, Rage akiwa nchini Sudan kwenda Marekani, aliamua kuahirisha safari hiyo, mara moja na ameamua kupanda ndege kurejea nchini ambapo atatua leo jioni.
Imeelezwa Rage amepanga kupokewa na wanachama wanaomuunga mkono ambao watakwenda naye kwa maandamano hadi makao makuu ya klabu ambako atafanya mkutano.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Swedi Nkwabi, alisema: “Sisi tunaamini tulichoamua ni sahihi, kama mzee Kilomoni amesema tungeweza kumuonya, kweli yuko sahihi lakini katiba inaturuhusu kuchagua pia kama kumuonya au tunaona kumsimamisha ni sahihi, pia hakuna tatizo.”

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

NINI MAANA YA MAPENZI

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU