YANGA WATANGULIA LAKINI JE WALIFIKA?
Ama kweli kutangulia si kufika,au kama wanavyosema wakongomani kuwa KOKENDE LIBOSO,EZA KOKOMATE.
Usemi huo ulidhihirika hapo jana kwenye uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya Mabingwa watetezi Ligi kuu soka
Tanzania Bara Timu ya Yanga,pamoja na kutangulia kufunga bao 3 dhidi ya
Simba hadi mapumziko,walijikuta wakiambulia sare ya bao 3-3 hadi Mwisho
wa mchezo baada ya Simba kusawazisha bao zote katika Kipindi cha Pili.
Lango la Simba lilikuwa matatani tena katika dakika ya 35 pale Mganda Khamis Kiiza alipoandika bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia baada ya mpira uliorushwa na Mlinzi Mbuyu Twite kuparazwa kichwa na Didier Kavumbagu kabla ya kumkuta Mfungaji aliyeujaza wavuni.
Mganda huyo Khamis Kiiza almaaruf Diego aliandika bao la tatu kwa Yanga sekunde chache kabla ya Mapumziko kufuatia kazi nzuri ya Haruna Niyonzima alieyekokota mpira na kumpasia Didier Kavumbagu ambaye naye alimsogezea Mfungaji.
Huku Mpira ukienda Mapumziko Yanga wakiongoza kwa bao 3-0 ,baadhi ya mashabiki wa Simba walianza kuondoka uwanjani kwa kukata tama hasa kutokana na kiwango duni cha mchezo kilichoonyeshwa na timu yao,huku Mashabiki wa Yanga wakishangilia na kuwadhihaki Simba kwa kuonyesha kuwa wangeweza kulipiza kichapo cha bao 5-0 walichoshushiwa na Simba mwaka jana kwenye uwanja huo huo wa Taifa.
Kipindi cha Pili kilianza kwa Simba kuwapumzisha Abdul halim Humoud na Haroun Chanongo na kuwaingiza Said Ndemla na William Lucian,katika idara ya Kiungo,mabadiliko ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo hasa yaliyobadili sura ya mchezo baada ya idara ya kiungo ya Yanga kuanza kuzidiwa na kasi ya vijana hao ambapo katika dakika 53 Betram Mwombeki aliipatia Simba bao la kwanza baada ya pasi ya Mrundi Khamis Tambwe.
Dakika tatu baadae Mpira wa Kona uliopigwa na Ramadhan Singano ulimkuta Joseph Owino ambaye aliujaza wavuni na kuipatia Simba bao la Pili lililozidi kuwapa morali wachezaji na mashabiki waliokuwa wameamka upya.
Hatimaye Simba wakaweza kusawazisha katika dakika ya 83 kufuatia Beki Kaze Gilbert kujitwisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mlinzi Nassor Masoud Chollo.
Kwa Matokeo hayo Simba sasa inashika nafasi ya tatu kwa kuwa Pointi 19 nyuma ya Azam na Mbeya City zenye pointi 20 kila moja lakini Simba imecheza mechi moja pungufu.
Nao Mabingwa watetezi Yanga wako nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 16.
Hakika lilikuwa Pambano ambalo Yanga walijiamini
kuwa wameshinda kwa kutangulia kuongoza bao 3-0 ambalo si kawaida
katika mechi za watani hao wa jadi katika Soka la Tanzania,na ndiyo
Maana Simba walishangiliwa kwa nguvu kana kwamba wameshinda baada ya
Kutoka nyuma na kusawazisha bao tatu.
Kwa upande mwingine mashabiki wengi walianguka
na kuzimia ama kwa kushangilia matokeo au mshtuko kutokana na kutoamini
kilichokuwa kinaendelea uwanjani hapo.
Kwa upande mwingine kukamilika kwa mechi hiyo
kunafanya maisha yaendelea kama kawaida baada ya tambo za kila upande
kwa takriban zaidi ya wiki moja ambapo mashabiki wa pande zote walikuwa
wakitambiana kuwa kila mmoja timu yake ingeshinda Pambano hilo ambalo
kwa kawaida huwagawanya mashabiki wa nchi hii pande mbili.
Comments
Post a Comment