MBEYA CITY KUITIKISA NCHI KWA SAA KADHAA LEO?, WAWATETEMESHA JKT RUVU SOKOINE, MAKATA AWATULIZA MZUKA!!


                                                                 
“Tunataka kuwaambia Watanzania kuwa klabu yetu ni mpya na ina falsafa mpya kabisa, vijana ndio msingi wetu. Pia tunajua mashabiki ni mchezaji wa 12, tunawaomba wajitokeza leo kwa wingi kwani tutawapa raha kama tulivyofanya huko nyuma”. Alisema Maka.


WAKALI wapya wa ligi kuu soka Tanzania bara `Nyuki wa nyanda za juu kusini`, klabu ya Mbeya City wametamba kuwa leo wanataka kuisimamisha nchi kwa muda na kuwajulisha watanzania kuwa falsafa yao mpya na mtazamo mpya kweli unafanya kazi.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Mbeya na mtandao wa Samwelmlawa muda mfupi uliopita, Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Maka Mwalwisyi amesema wachezaji wote wana morali kubwa na wanategemea kuiambia Tanzania kuwa falsafa mpya imekuja na watapa matokeo mazuri jioni ya leo dhidi ya JKT Ruvu na kuongoza ligi kwa saa kadhaa.
“Falsafa na mtazamo mpya ndio dira yetu, sisi tunaamini kuwatumia vijana wadogo, tunawafundisha na kuwakumbusha vipaji vyao, watu wengi wanajua ni nguvu ya soda, lakini watashanga tulivyoanza ndivyo tutakavyomaliza”. Alisema Maka.
IMG_2090
Mbeya City, `Nyuki wa nyanda za juu kusini` wanaendelea na mpango wao wa kuwatoa watu nishai, na leo hii kibaruani na JKT Ruvu uwanja wa Sokoine
Maka alisema wanawaheshimu sana JKT Ruvu kwani wana mwalimu mzuri aliyefanya kazi
Mbeya, hivyo wanauchukulia kwa umuhimu mkubwa mchezo huo ambao wakishinda watafikisha alama 20  na kama Azam fc atafungwa au kutoa sare leo hii jijini Arusha dhidi ya JKT Oljoro, basi Mbeya City watapanda kileleni wakisubiri matokeo ya kesho Simba na Yanga uwanja wa Taifa.
SONY DSC
JKT Ruvu, `Ingoma inogile`, wapo kibaruani kuwakabili Mbeya City
Kwa upande wa kocha mkuu wa JKT Ruvu, Mbwana Makata amesema anajua mchezo utakuwa ni mgumu, na anajua City wanawaza kivyao na wao kivyao, lakini wasitegemee mtelemko kabisa kutokana na mazoezi waliyofanya kujiandaa kuwakabili.
“Wachezaji wangu wako vizuri na tunategemea kufanya vizuri, ni kweli tumeteteleka kidogo kwa mechi za nyuma, lakini cha msingi ni kuelewa kuwa ligi ni ngumu na kuna changamoto nyingi za kiushindani, hivyo mashabiki wasikate tamaa”. Alisema Makata.
Hata hivyo tangu ligi imeanza, Mbeya City walishinda mechi moja tu dhidi ya Ruvu Shooting (mabao 2-1) kati ya nne walizocheza katika uwanja wao wa nyumbani wa kumbukumbu ya Sokoine.
Walianza kwa suluhu dhidi ya Kagera Sugar, wakatoka sare ya 1-1 na Yanga, wakashinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting,na wakatoa sare ya 1-1 na Coastal Union, kabla ya kusafiri kwenda nje.
Ugenini walianzia Manungu ambako walitoka suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar, wakatoka 2-2 dhidi ya Simba SC uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, wakashinda 2-1 Sh. Amri Abeid Arusha dhidi ya JKT Oljoro, wakasafiri mpaka Tabora na kuwafunga Rhino Rangers mabao 3-1 na wakamalizia Tanga ambapo waliwafunga Mgambo JKT bao 1-0, na hatimaye leo wamerejea tena nyumbani dhidi ya JKT Ruvu.
Kwasasa City wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 17 sawa na Azam fc ambao wako nafasi ya pili, lakini wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, na juu yao yupo Simba mwenye pointi 18.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Oljoro JKT na Azam (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Mtibwa Sugar na Mgambo Shooting (Uwanja wa Manungu, Turiani), Ashanti United na Ruvu Shooting (Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam) na Kagera Sugar dhidi ya Coastal Union (Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba).
Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea katika viwanja nane leo (Oktoba 19 mwaka huu) huku Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ukiwa mwenyeji wa mchezo kati ya African Lyon na Friends Rangers.
Nayo Villa Squad itacheza na Green Warriors katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Polisi Morogoro na Kimondo (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Lipuli na Kurugenzi (Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa) na Mkamba Rangers dhidi ya Majimaji (Uwanja wa CCM Mkamba, Morogoro).
Toto Africans na Mwadui (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Polisi Dodoma na Polisi Tabora (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), wakati Polisi Mara na pamba zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

NINI MAANA YA MAPENZI