MAMA LULU ATOBOA SIRI ZA KANUMBA
Mama wa staa wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Lucresia Karugila kwa mara ya kwanza amemfungukia marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, 2012.
Marehemu Steven Kanumba.
Katika mahojiano rasmi na Risasi Jumamosi, juzi jijini Dar, Mama Lulu
aliweka wazi kila kitu kuhusu madai mbalimbali ya yeye na mama Kanumba,
Lulu na marehemu Kanumba.Mambo yaliyoelekezwa ayajibu mwanamama huyo ni pamoja na madai kwamba alishapokea barua ya posa ya Kanumba kutaka kumuoa Lulu
, yeye na mama Kanumba kugombana hivi karibuni na Lulu kumjali zaidi mama Kanumba kuliko yeye.
Awali, mwanamke huyo alisema miongoni mwa watu waliofiwa na Kanumba yeye yupo mstari wa mbele kwani uchungu alioupata siku ya tukio mpaka leo haujamtoka.
Mahojiano kamili yalikuwa kama ifuatavyo:
Risasi: Mama kuna madai kadhaa ambayo ni vyema uyajibu.
Mama Lulu: (Kwa ukali kidogo) maswali gani? Mimi sitaki waandishi, nilishasema! Kama ni kuhusu Lulu muulizeni mwenyewe.
Ilibidi waandishi watumie kazi ya ziada ili mama huyo aweze kuzungumza.
Risasi: Ni mambo ya kawaida tu mama, wewe ndiyo unafaa kujibu, tafadhali tusikilize.
Mama Lulu: Haya, ulizeni.
ALIUJUA UHUSIANO WA KANUMBA NA LULU?
Risasi: Kuna madai kwamba uliujua uhusiano wa kimapenzi kati ya Lulu na Kanumba, lakini mama Kanumba alikuwa hajui kinachoendelea, ni kweli?
Mama Lulu: Kwanza katika maisha yangu hakuna siku niliyowahi kupata mshtuko kama niliposikia Kanumba amefariki dunia na mwanangu Lulu kahusishwa na kifo kile, nilishtuka sana.
“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kujua kumbe Kanumba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanangu Lulu, lakini kabla ya hapo sikuwa najua lolote.
ALIMKABIDHI LULU KWA KANUMBA
“Ninachoweza kukiweka wazi ni kwamba, nilikutana na Kanumba nikamkabidhi mwanangu kwa moyo mweupe amlee kisanii kwa sababu nilijua anaweza, kumbe na wao wakaanzisha uhusiano huo kwa siri.
KWA NINI ALIMKABIDHI LULU KWA KANUMBA?
“Mimi na Kanumba tulikuwa tumezoeana sana. Alinipa heshima zote kama mama yake na alikuwa kijana mwenye aibu kwangu kutokana na heshima, haikuwa rahisi kuangaliana machoni na ndiyo maana niliamua kumpa Lulu amkuze kisanii.
ALIPOKEA BARUA YA POSA YA KANUMBA?
“Si kweli, sijawahi kuona wala kupokea barua ya posa ya Kanumba kumchumbia Lulu.
KAMA KANUMBA ANGETAKA KUMUOA LULU
“Lakini nataka kusema kwamba kama Kanumba angekuwa hai na angetaka kumuoa Lulu ningefurahi sana kwani naamini mpaka sasa wangekuwa wamepata mtoto mzuri na sisi wazazi tukaitwa bibi.”
MADAI YA KUGOMBANA NA MAMA KANUMBA
Risasi: Kuna madai kwamba wewe na mama Kanumba kwa sasa ni paka na panya, na sababu kubwa ni Lulu kumjali zaidi mwanamke huyo kuliko wewe, ni kweli habari hizi?
Mama Lulu: Mimi na mama Kanumba hatuwezi kugombana hata siku moja. Kwanza Lulu nimempa jukumu kwamba kwa sababu wote ni mama zake, akinunua nyama kilo tano kwa ajili yangu na kwa mama Kanumba apeleke tano.
“Akinunua vocha ya elfu tano kwangu na mama Kanumba amtumie kama hiyohiyo. Kwa hiyo hakuna ugomvi.”
Risasi: Je, Lulu akimzidishia mama Kanumba wewe hutajisikia vibaya?
Mama Lulu: Siwezi kujisikia vibaya ingawa mimi kwa sababu naishi naye ni lazima nitapata zaidi, lakini akimsaidia naona ni sawa tu.
ALIKUWA AKIMUOGOPA MAMA KANUMBA
Mwandishi: Ilikuwaje ukakutana na mama Kanumba kwa mara ya kwanza?
Mama Lulu: Lulu ndiye aliyekuwa akinishawishi kila mara niende nikaonane na mama Kanumba ingawa wakati mwanangu yuko jela kiukweli nilikuwa namuogopa sana.
“Unajua yule aliyepotea (Kanumba) ni mtoto kama wangu, lakini alipotoka tulikwenda nyumbani kwake na tunamshukuru alitupokea vizuri. Awali kabla ya kifo cha Kanumba sikuwahi kufahamiana naye.
Risasi: Ukiambiwa uongee na Watanzania utataka kuwaambia nini?
Mama Lulu: Cha kuwaambia ni kwamba, mimi na mama Kanumba si marafiki bali ni mtu na dada yake. Nawaomba wawaombee mama Kanumba na Lulu mwenyewe ili waendelee kupatana na kufanya kazi za sanaa pamoja kama walivyoanza.
Risasi: Tunashukuru sana mama.
Mama Lulu: Karibuni sana, mimi huwa naogopa sana magazeti, sipendi sana kuongea na waandishi wa habari.
KUMBUKUMBU YA LULU
Katika mahojiano na kipindi cha Take One kinachorushwa na Clouds TV, Lulu alisema: “Katika maisha yangu sitakaa nimsahau Kanumba kwa sababu alikuwa ni zaidi ya mpenzi. Kamwe sitamsahau.”
Comments
Post a Comment