YANGA YAKAZIWA NA MBEYA CITY , YALAZIMISHA SARE YA 1-1, MNYAMA ATAFUNA MIWA YA MTIBWA TAIFA, AZAM WAPONEA CHUPUCHUPU KAITABA, JKT RUVU WAZIDI KUPAA KILELENI!!


MZUNGUKO wa tatu wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 umeendelea kushika kasi leo hii kwa timu zote 14 kushuka katika viwanja saba tofauti nchini.
Mabingwa watetezi, klabu ya Yanga ya Dar es salaam wameponea chupuchupu mbele ya Wenyeji wa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, klabu ya Mbeya  City ambapo wamelazimishwa  sare ya 1-1, huku wakishuhudiwa na mwenyekiti wake Yusuf Manji aliyewasili leo mchana.
Mbeya City wanaofundishwa na Juma Mwambusi ndio walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 49 kupitia kwa Mwagane Yeyah na Yanga walisawazisha bao hilo katika dakika ya 71 kupitia kwa Mrundi, Didier Kavumbagu “Kavu”.
Mbeya City walianza kwa kasi mchezo huo huku wakionana kwa pasi safi na kushambulia lango la Yanga kama Nyuki, lakini makosa ya washambuliaji yaliwanyima mabao ya wazi.
DSC00396 
Lakini...
katika mechi ya leo kumetokea mambo ambayo si ya kiungwana katika mchezo wa soka.
Mapema wakati Yanga wakiwasili uwanjani na basi lao, mashabiki wa Mbeya City walilirushia chupa za maji na mawe na kusababisha kioo cha mbele upande wa dereva kuvunjika.
Suala hili limetafsiriwa na wadau wa soka kuwa ni kukosa busara kwa mashabiki ambao hawakuwa na sababu ya msingi kulishambulia basi la Yanga.
Lakini kali zaidi ilikuwa ni mayai matatu yaliyochorwa kwa rangi nyekundu na penseli ambayo yaliokotwa na meneja wa uwanja wa sokoine Modestus Mwaluka katikati ya uwanja na kuzua wasiwasi kwa watu waliokuwepo uwanjani.
38Wataalamu wa mambo ya sayansi ya asili wameelezea suala hilo kuwa ni imani za uchawi na ushirikina katika soka la Tanzania, lakini mayai hayo yameshindwa kuwapa ushindi Yanga na Mbeya City kwani haijulikani ni timu gani aliyaweka dimbani.
Kwa upande wa meneja Mwaluka alikataa kuelezea chochote juu ya Mayai hayo zaidi ya kusema yeye aliitwa kuwa kuna mayai yapo katikati ya uwanja na ameenda kuyatoa bila kujua nani aliyaweka nay a kazi gani.
Baada ya mechi hiyo, kocha mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema tatizo kubwa la kikosi chake ni safu ya ushambuliaji kukosa magoli ya wazi.
“Kila tunavyozidi kusonga mbele, kikosi kinaimarika na kuonesha soka zuri. Tunajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar Ugenini, nimeshayaona matatizo ya safu yangu ya ushambuliaji ,naenda kuyafanyia kazi”. Alisema Mwambusi.
Kwa upande wa kocha wa Yanga, Ernie Brandts amekiri kukerwa na sare ya pili na kusema leo hii aliamua kutumia washambuliaji watatu, Didier Kavumbagu, Hussein Javu na Said Bahanuz kwa lengo la kupata mabao, lakini alisahau kuweka mipango katika safu ya kiungo na ulinzi.
“Mechi ilikuwa nzuri, sikutegemea sare, lakini wapinzani wetu wamecheza vizuri na nawaheshimu kwa uwezo wao. Binafsi kupata sare ya pili sijapenda, ila najipanga kwa mechi zijazo”. Alisema Brandts.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan/Jerry Tegete dk59, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Hussein Javu na Said Bahanuzi/Oscar Joshua dk59.
Mbeya City; David Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Antony Matogolo, Yohana Morris, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul Nonga/Fidelis Castor dk82, Deus Kaseke, Yussuf Willson/Alex Sethi dk 59.
1174988_407014929399504_1366482008_nMechi nyingine, wekundu wa Msimbazi Simba wameendeleza wimbi la ushindi baada ya leo hii kuwatungua Mtibwa Sugar mabao 2-0 huku mabao ya Mnyama yakifungwa na Henry Joseph Shindika dakika ya 70 na Betram Mombeki katika dakika ya 90.
Wana lambalamba Azam fc wameponea chupuchupu mbele ya Kagera Sugar baada ya kulazimisha sare ya 1-1 katika dimba la Kaitba.
Huko  Mkwakwani Tanga, Wagosi wa Kaya Coastal Union wamelazimishwa suluhu ya bila kufungana na maafande wa Tanzania Prisons “Wajelajela”.
simbaNao Ruvu Shooting wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo JKT, huku bao la watoto hao wa Boniface Mkwasa likifungwa na Elias Maguli.
Maafande wa JKT Olojoro wamebanwa katika dimba lao la nyumbani la Sh. Amri Abeid jijini Arusha baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers ya Tabora.
Wakati huo huo, Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuwatungua Ashanti United bao 1-0  katika uwanja wa Azam Complex na kujikita zaidi kileleni wakiwa na pointi 9 huku wakifuatiwa na Simba Sc wenye pointi 7 katika nafasi ya pili.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

NINI MAANA YA MAPENZI

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU