JESHI LA POLISI LATEUA ASKARI WA KUMFUATA AGNESS MASOGANGE ALIYENASWA NA MADAWA YA KULEVYA AFRIKA KUSINI
Jeshi la Polisi litapeleka askari wake Afrika Kusini kuwahoji washiriki wa video za wasanii wa muziki wa Bongo fleva, Agnes Gerald ‘Masogange’ na mwenzake Melisa Edward waliokamatwa nchini humo na dawa za kulevya.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa aliiambia Mwananchi kwa simu jana kuwa watawapeleka polisi kuwahoji na wanaamini wahusika watawaeleza wahusika wa mzigo huo.
Wasichana hao walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini wakitokea Tanzania wakiwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine.
“Tutawapeleka askari wetu kuwahoji, tumekwishaanza uchunguzi wa hili...wote watakaohusika katika hili tutawakamata, lakini tunakwenda polepole hatua kwa hatua kuhakikisha tunawanasa wahusika sahihi,” alisema Nzowa.
Naye Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, (JNIA), Moses Malaki alieleza kushangazwa na kiasi kikubwa kupitishwa kwenye uwanja huo licha ya kuwa wapo watu wenye dhamana ya kuangalia usalama.
“Sitaki kusema tutafanya nini, lakini ninachotaka kukwambia ni kwamba uchunguzi umeanza na suala zima tumewaachia polisi na sisi tutatoa ushirikiano kwa kila hatua watakayotutaka, lazima kukomesha hili.
“Tutaangalia nani walikuwa zamu siku hiyo,” alisema Malaki.
Comments
Post a Comment