WANAOAMINI, NDIYO WANAOONGOZA KWA KUSALITI WENZAO, UPO?


AWALI ya yote nimshukuru Mungu kwa kunifanya kuwa miongoni mwa wale waliobahatika kuuona mwaka huu wa 2014 tukiwa wazima. Nichukue nafasi hii pia kuwatakia kila la kheri nanyi ili wote tuwe na amani na furaha.
Mpenzi msomaji wangu, kilio cha wengi walio kwenye uhusiano ni kuhisi wanasalitiwa na wapenzi wao waliotokea kuwaamini sana. Wapo ambao si tu kwamba wanahisi bali wanawafumania kila kukicha waume/wake zao licha ya imani waliyokuwa wamejijengea kuwa kwa mapenzi wanayooneshwa hawawezi kusalitiwa.

Imefika wakati baadhi yetu hatutaki hata kufuatilia nyendo za wenza wetu tukijua kwamba kufanya hivyo ni kujitafutia presha za bure.
Kwa kifupi kasi ya wapenzi kusalitiana imekuwa ikiongezeka kila siku kiasi cha baadhi kuhisi bila kusaliti hawasikii raha. Yaani wanapatiwa kila kitu na wenza wao lakini bado wanatoka nje.
Unakuta mwanaume ana mke mzuri anayejua mapenzi na kila kitu lakini bado mwanaume huyo haridhiki. Pia wapo wanawake ambao wamebahatika kuwapata wanaume ‘handsome’, wanaojua mapenzi na kujali pia lakini bado tamaa za usaliti wanakuwa nazo. Ukiuliza kipi kigeni wanachofuata huko nje, jibu hakuna.
Nilishawahi kufanya uchunguzi huko nyuma kwa kuzungumza na baadhi ya wanawake walio kwenye ndoa kuhusu hili suala la kusalitiwa. Wengi walikiri kujua kwamba waume zao wanawasaliti lakini wenyewe wanadai ni mambo ambayo wakiyafuatilia hawawezi kudumu kwenye ndoa zao.
“Hivi unadhani ni wakati wa kuamini asilimia zote kwamba husalitiwi? Binafsi kwa ninavyomjua mume wangu na huu utitiri wa wanawake ‘cheap’ huko mtaani, najua anachepuka ila kinachonifanya niwe na amani ni kwamba, ananiheshimu na sijawahi kumfumania.
“Hilo ndilo linalonifanya niwe mpole ila najua hakosi mwanamke mwingine na nikimfuatilia najua nitamfuma tu,” alisema mama Faraja wa Kinondoni jijini Dar ambaye ndoa yake sasa ina miaka 12.
Mwingine ambaye nilibahatika kuzungumza naye alijitambulisha kwa jina la Husna wa Kimara jijini Dar.
Huyu anaeleza kuwa, amekuwa akishuhudia wanaume wengi anaowajua wakizisaliti ndoa zao hivyo kwake ni vigumu kuamini kwamba mume wake hamsaliti.
“Huwa nawaona wanaume ambao sikuwahi kufikiria kuwa wanaweza kuwasaliti wake zao lakini wanafanya hivyo. Mfano kuna shemeji yangu, mke wa rafiki yangu, ni mpole sana, mtaratibu na anaonekana asiye na ‘time’ na mademu.
“Mchumba wake naye alikuwa akimuamini sana kiasi cha wakati mwingine kuturingishia kuwa amepata mume mtulivu. Huwezi kuamini siku moja nilimfuma akiingia gesti na kidemu. Nilipigwa na butwaa na hapo ndipo nilipoamini kwamba hakuna asiyesalitiwa.”
Hao ni wanawake wachache tu ambao niliongea nao lakini wengi walikiri usaliti upo tena wanaoongoza kusaliti ni wale ambao wake zao wanawaamini sana. Kuna wanawake ambao walifikia hatua ya kukiri kwamba eti kwa kuwa wamebaini waume zao wanawasaliti basi nao wanalipiza kisasi bila kujua kuwa wanajitafutia matatizo zaidi.
Hii yote inaonesha ni kwa jinsi gani mapenzi ya sasa usaliti unachukuliwa kama fasheni. Yaani mama fulani akimuona shoga yake ana ‘kiserengeti boy’ basi naye anatafuta ili waende sawa. Huu ni ulimbukeni uliopitiliza.
Kipi kifanyike?
Kutokana na utafiti huu niliofanya ambao naamini hata wewe unakubaliana nao, kuna kila sababu kila aliye kwenye uhusiano kumuamini mwenza wake kwa kiwango kinachostahili.
Sisemi umuamini tu hata kama unaona anakuchezea rafu, la hasha! Muamini pale ambapo una sababu ya kufanya hivyo.
Ukiona dalili za wazi kwamba anakusaliti, ukafuatilia na kugundua ni kweli ana mtu au watu wengine unaochangia nao penzi, hutakiwi kuvumilia. Mtu huyo atakuwa hana nafasi kwenye maisha yako hivyo haraka muweke kando.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

NINI MAANA YA MAPENZI