HUNA SABABU YA KUUWEKA MOYO WAKO REHANI!

MAPENZI ni sanaa yenye wigo mpana sana. Unahitajika uwe mbunifu sana ili uweze kuendelea kuwa bora kwa mpenzi wako kila siku. Lazima uwe mtafutaji wa kitu kipya ili uweze kuwa wa tofauti kwa mwenzako.

Huwezi kuwa yuleyule, ikiwa hivyo maana yake utakinaiwa. Naam! All About Love ni safu nzuri kwako kwa ajili ya kuongeza maarifa na kukufanya uendelee kuwa bora zaidi kwa mpenzi wako.
Ndugu zangu, mapenzi ni furaha. Huna sababu ya kujitafutia huzuni kwenye mapenzi. Ni ukweli ulio wazi kuwa, kung’ang’ania mahali usipopendwa au kulazimisha penzi sehemu usiyotakiwa maana yake kuuweka moyo wako rehani kwa ajili ya mateso baadaye.
Nitafafanua kwa mapana, maeneo ambayo kwa hakika kuendelea kung’ang’ania ni kuweka moyo rehani. Hebu twende tukaone.
WALIO KWENYE NDOA
Asikudanganye mtu, mume/mke wa mtu sumu! Fanya ujanja wako uwezavyo, jifanye muhuni unavyoweza lakini si tabia njema kutoka na mtu ambaye ana mwenza wake tena wa ndoa.
Hebu jiulize, kama ingekuwa ni wewe ungejisikiaje? Ukisikia mkeo anatoka na mwanamke mwingine utajisikiaje? Au pengine umeolewa, halafu ukasikia au kupata uhakika kuwa mume wako anatoka na mwanamke mwingine utajisikiaje? Achana na hilo, unajiweka kwenye hatari kubwa, mwenye mali atakapogundua.
WENYE WAPENZI
Katika hali ya kawaida kabisa, unawezaje kumtaka mtu ambaye tayari unajua ana mtu wake? Busara hapo iko wapi? Ukijichunguza kwa makini lazima utagundua kwamba una tatizo.
Mtu ambaye tayari ana mpenzi wake, maana yake ni kwamba amefika; kitendo cha kumtongoza, kinaonesha ni kwa kiwango gani umejaa tamaa ambazo ndizo zinazokuongoza, maana kwa busara huwezi kumtaka mtu ambaye ana mpenzi wake.
Jambo la kusha-ngaza zaidi ni kwamba, kuna wengine wana-ambiwa wazi kuwa wana watu wao, lakini ndiyo kwanza mtu anaendelea kulazimisha, tena akitoa ahadi kedekede ili ampate. Huo ni ujinga usio na maana.
JIFUNZE HAYA
Kwa bahati mbaya, wanapokutana wote wa ‘hovyo’ wanajikuta wameingia kwenye mapenzi. Hebu jiulize wewe ambaye umeingilia penzi la mtu, akili yako inafanya kazi sawasawa kweli?
Unawezaje kuingia kwa mtu ambaye tayari ana wake? Kuna vitu kadhaa vya kujifunza hapa. Kwanza lazima utambue kuwa, huyo ambaye amekubali kuwa na wewe wakati huohuo ana mwingine, maana yake hana penzi la dhati.
Si ajabu akiwa na wewe, akatafuta kuwa na mwingine pembeni yako! Hekima iko wapi? Kuna tatizo gani kusubiri mwingine ambaye atakuwa wako peke yako? Tatizo wengi wanachukulia mapenzi kama maigizo tu. Hawaoni umuhimu wala thamani ya kupenda kwa penzi la kweli.
Lazima uwe na msimamo katika maisha yako. Siyo sifa kuwa na wapenzi wengi au kuingia kwenye uhusiano wa mwingine. Unadhani mwenzako anaumia kwa kiasi gani? Vipi kama na wewe ukija kuingiliwa na mtu mwingine?
Unahitaji kutulia na kuijua thamani yako, halafu kuacha tamaa ambazo hazina maana. Ni sifa njema kuwa na mwenzi wako peke yako bila kuchangia na mwingine. Hilo litawezekana kwako kama nawe utaacha tabia ya kuingia kwenye uhusiano wa wengine.
TAFUTA TIBA
Tabia hiyo ni tatizo. Kama unayo unatakiwa ujue kwamba ni ugonjwa na unatakiwa kuushughulikia mapema iwezekanavyo. Mtu ambaye anaishi kwa kuongozwa na mapenzi ya kweli, hawezi kukubali kuwa na mtu ambaye ana mwezi wake. Kufanya hivyo ni kuuweka moyo wako rehani.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

NINI MAANA YA MAPENZI