BABU WA LOLIONDO TENA!
:
MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Ambilikile Mwaisapila ‘Babu wa Loliondo’ amesema Mungu ameendelea
kujifunua kwake na kumuonesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na
baadaye kioo cha dunia. Ametoa kauli hiyo Septemba 24, mwaka huu mbele
ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha
Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu
uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini
Arusha. Mchungaji Mstaafu Mwaisapila aliyesifika kwa tiba ya kikombe cha
dawa, alisema kuna mambo mengi ambayo.. yameandikwa kwenye Biblia na
hayakutokea Israeli sasa yatafanyika Samunge. “Mungu ametupenda sana,
yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na
nimeyaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku
akishangiliwa. Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa
kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa
hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa misaada iliyotoa
wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi. Pamoja na
maono hayo aliyopewa Babu wa Loliondo, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa
la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT), marehemu Moses Kulola
alikuwa akimpiga waziwazi katika mahubiri yake akidai mwenendo wa tiba
alizokuwa akizitoa hazifanani na mafundisho ya Mungu. Kama hiyo
haitoshi, watumishi mbalimbali wa Mungu wamekuwa hawamuamini. Askofu
Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe na
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’
kwa nyakati tofauti waliwahi kunukuliwa wakisema hawana imani na tiba ya
kikombe iliyokuwa ikitolewa na Babu wa Loliondo
Comments
Post a Comment