PENZI LISILOISHA 2

Kijana mdogo, Jafet ambaye alikuwa amehitimu darasa la saba na kufaulu vizuri kuendelea na masomo ya sekondari, anajikuta akikwama kuendelea na masomo kutokana na ufukara wa kupindukia wa wazazi wake. Hali hiyo inamuumiza sana Jafet hasa anapoona wenzake wameanza kwenda shule, muda wote anashinda akiwa analia na kujiinamia kwa huzuni.
Mama yake aliyekuwa akijishughulisha na kazi ya kufanya vibarua vya kupalilia mashamba ya mihogo ili apate chakula cha yeye na familia yake, naye anaumizwa sana na hali aliyokuwa nayo mwanaye. Baada ya kumlalamikia na kumlilia sana, mwanamke huyo maskini anaamua kumsaidia mwanaye.
Kwa bahati nzuri, anakutana na shoga yake waliyekuwa wakifanya naye vibarua ambaye anamuelekeza kwenda kwenye ofisi za mapadri wa Kijiji cha Rwamgasa, Geita ambako anakutana na padri mzungu, Brocco Giovanni anayeahidi kumsaidia. Anamuagiza kwenda kumleta mtoto huyo ili azungumze naye na kumpa masharti yaliyokuwa yanatakiwa.Je, nini kitafuatia?
Usiku huo ulikuwa mrefu sana kwa Jafet, hata usingizi haukuja, muda
wote alikuwa akiwaza safari ya kwenda kuonana na mapadri kisha kwenda kuanza masomo ya sekondari. Alfajiri na mapema, Jafet alikuwa wa kwanza kuamka, akawasha kibatari na kwenda nje kuoga, muda mfupi baadaye akawa anajiandaa.
Akavaa kaptura yake aliyokuwa akiitumia kama sare wakati akisoma shule ya msingi, ambayo ndiyo nguo nzuri pekee aliyokuwa nayo, nyingine zilikuwa na viraka vingi, hali iliyomfanya aone aibu kuzivaa.“Mh! Umewahi sana kuamka leo,” mama yake alimwambia baada ya kumkuta ameshatoka nje huku kukiwa bado hakujapambazuka. Baada ya mama yake kumaliza kujiandaa, walitoka na kuianza safari ya kuelekea kwenye ofisi za mapadri za Rwamgasa Parish.
Wakati wanaondoka, baba yake alikuwa bado akikoroma kutokana na usingizi mzito uliosababishwa na pombe nyingi alizokunywa jana yake usiku.Walitembea kwenye umande, wakikatiza kwenye mashamba ya watu na baada ya safari ndefu, hatimaye waliwasili kwenye ofisi za mapadri na kupokelewa na wahudumu waliokuwa wakifanya usafi kwani ofisi bado zilikuwa hazijafunguliwa.
Ilibidi wakae na kusubiri ambapo baada ya muda, ofisi zilianza kufunguliwa, Jafet na mama yake walikuwa ndiyo wa kwanza kuingia. Wakaenda kuonana na Padri Brocco ambaye alionesha kuvutiwa na uelewa mkubwa aliouonesha Jafet wakati akihojiwa maswali mbalimbali na padri huyo.
Baada ya mazungumzo marefu, hatimaye walikubaliana kwamba mapadri watasimamia kila kitu kuanzia sare za shule, vifaa vya kusomea, mavazi na fedha za kujikimu kwa muda wote ambao Jafet atakuwa anasoma.
“Kwani ataenda kusomea wapi?”
“Tutampeleka kwenye Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kwimba, Mwanza inayomilikiwa na kanisa,” alisema Padri Brocco huku akimsisitiza Jafet kwenda kusoma kwa bidii.Kutokana na furaha aliyokuwa nayo Jafet, alijikuta akishindwa kuyazuia machozi yasimtoke na kuulowanisha uso wake wa kitoto. Hatimaye waliondoka ofisini hapo kwa makubaliano kwamba siku tatu baadaye, wampeleke Jafet akiwa tayari kwa safari ya kuelekea shuleni.
Njia nzima Jafet alikuwa akichekacheka mwenyewe kama mwendawazimu akiwa haamini kwamba hatimaye kilio chake cha siku nyingi kilikuwa kimepatiwa ufumbuzi. Alipofika nyumbani kwao, hakutaka kukaa ndani, alianza kupita mitaani kwa marafiki zake na kuwahadithia juu ya safari yake ya kwenda shule.
Baba yake aliporejea kutoka kwenye pombe zake, alipewa taarifa kuhusu hatua hiyo lakini hakuonekana kujali sana zaidi ya kwenda kujitupa kwenye kitanda cha kamba, akapitiwa na usingizi mzito.Hatimaye siku iliwadia ya Jafet kwenda kuripoti kwenye ofisi ya mapadri, akapelekwa na mama yake huku akiwa amebeba mfuko wa plastiki uliokuwa na nguo zake kadhaa zilizochakaa. Akakabidhiwa kwa mapadri ambapo ilimlazimu kulala hapo wakati akitafutiwa nguo nzuri na vifaa vingine kwa ajili ya shule. Kesho yake safari ikaanza kuelekea Kwimba shuleni.
Jafeti, Padri Brocco na wanaume wengine wawili, walisafiri kwa gari la mapadri hao mpaka jijini Mwanza ambako alipelekwa moja kwa moja mpaka shuleni, akakabidhiwa kwenye uongozi wa shule hiyo na kuyaanza rasmi maisha mapya ya shuleni.
Kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kusoma shule ya bweni, mara kwa mara alikuwa akikumbuka mno kurudi nyumbani kwao. Alishazoea kumuona mama yake na ndugu zake wengine kila siku lakini sasa hilo halikuwezekana.
Hata hivyo, kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele, alianza kuzoea mazingira ya shuleni. Akapata marafiki wapya waliomsahaulisha mambo ya nyumbani kwao. Kwa kuwa shuleni hapo kulikuwa na tofauti kubwa na nyumbani kwao, alijiapiza ndani ya moyo wake kusoma kwa bidii zote.
Juhudi zake zilianza kuonekana mapema kwani walipofanya mtihani wa kwanza wa nusu muhula (mid- term), Jafet alikuwa miongoni mwa wanafunzi watatu bora wa kidato cha kwanza. Licha ya umri wake mdogo, alikuwa na uelewa mkubwa darasani uliomfanya azidi kupata marafiki wengi wapya kila siku.
Siku zilizidi kusonga mbele huku Jafet akizidisha juhudi kwenye masomo. Hata muda wa likizo ndefu ya mwezi Juni ilipowadia, Jafet aliamua kubaki shuleni hapo kujisomea, hali iliyozidi kumuweka kwenye nafasi nzuri kimasomo.
Mpaka mwaka wa kwanza unaisha shuleni hapo, Jafet alikuwa amebadilika mno. Mafunzo ya kidini waliyokuwa wanapewa wanafunzi wote kila siku, yalimfanya kubadili mfumo wa maisha yake, dalili za upadri zikaanza kujionesha waziwazi kwama ilivyokuwa kwa wanafunzi wengi wa shule hiyo.
Upande wa darasani nako mambo yalizidi kumnyookea ambapo mpaka mwaka wa kwanza unaisha, yeye ndiye aliyeibuka mwanafunzi wa kwanza kwa matokeo ya jumla ya mwaka mzima, jambo lililowafurahisha sana mapadri waliokuwa wakimsomesha.
Hatimaye akaingia kidato cha pili huku akiendelea kuonesha juhudi kwenye masomo na tabia njema kwa wakubwa na wadogo. Hali hiyo iliwafanya wanafunzi wenzake karibu wote wampende na kumheshimu.
Kwa kuwa shuleni hapo pia walikuwa wanakula chakula bora, tofauti na kwao walikokuwa wanashindia mihogo ya kuchemsha na uji wa mtama uliotiwa chumvi, Jafet alinawiri. Mwili wake ambao awali ulikuwa ukionekana mdogo sana, ulibadilika na kuanza kutanuka. Siku zilizidi kusonga mbele huku akizidi kubadilika kila siku, akawa anazidi kukua kimwili na kiakili. Hatimaye mwaka wa pili nao uliisha, huku akiendelea kushikilia rekodi ya kufanya vizuri kuliko wanafunzi wenzake wote chuoni hapo.
Hatimaye aliingia kidato cha tatu ambapo alizidi kubadilika kimwili hasa kutokana na ukweli kwamba tayari alikuwa ameshaanza kubalehe, sauti yake ikabadilika na kuwa nzito huku ndevu zikianza pia kuota kwa mbali. Kama walivyo vijana wengi waliokamilika wanaopitia kipindi cha balehe, Jafet naye alianza kuwa na hisia za kimapenzi.
Hata hivyo, kutokana na mafunzo ya dini na nidhamu aliyokuwa nayo, kamwe hakuthubutu kuwaza kutafuta mpenzi hasa ukizingatia kwamba shule yao ilikuwa ni ya wavulana watupu na walikuwa wakiruhusiwa mara chache sana kwenda kutembea mjini.
Siku zilizidi kusonga mbele huku Jafet akianza kusumbuliwa na ‘ndoto nyevu’ nyakati za usiku, hali iliyozidi kumuweka kwenye wakati mgumu kihisia. Kutokana na jinsi alivyokuwa anaaminika shuleni hapo, alichaguliwa kuwa kiranja wa miradi, nafasi iliyokuwa inampa nafasi ya kwenda mjini mara kwa mara kufuatilia miradi mbalimbali ya shule.
Kutokana na kuzidiwa na hisia za kimapenzi zilizokuwa zinasababishwa na kipindi kigumu cha balehe alichokuwa anapitia, ilifika kipindi Jafet alijikuta akianzisha mazoea na msichana mmoja waliyekuwa wakikutana kwenye duka la dawa za mifugo alikokuwa anatumwa kwa ajili ya kwenda kununua dawa mbalimbali za mifugo ya chuo hicho.
“Mambo!”
“Poa.”
“Unaitwa nani mwenzangu maana leo siyo mara ya kwanza tunakutana.”
“Sitakutajia jina langu ila nasoma Shule ya Wasichana ya Bwiru,” alisema msichana huyo ambaye kiumri hawakuwa wamepishana sana na Jafet, mtoto wa kiume akaanza kushusha ‘mistari’.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA