PENZI LISILOISHA 1

Karibu kupata stori nzuri imeletwa kwenu na samwelmlawa fwatilia stori hii
Mama mimi nataka kuendelea na masomo ya sekondari.”
“Sasa mwanangu, unajua kabisa sisi wazazi wako hatuna uwezo, wewe unataka kwenda sekondari atakulipia nani ada?”
“Ina maana mimi huu ndiyo utakuwa mwisho wangu kielimu wakati nimefaulu? Mbona Alfayo mtoto wa mzee Maguha yeye anaenda sekondari?”
“Sasa wale wana mashamba, baba yake kauza shamba moja na ng’ombe ndiyo anamlipia ada, sisi wazazi wako tutauza nini? Hatuna shamba wala mifugo ya aina yoyote, sisi ni maskini mwanangu.”
“Mama mimi sikubali, nataka kwenda shule,” kijana mdogo, Japhet Lubongeja alikuwa akizungumza na mama yake lakini walishindwa kufikia muafaka, jambo lililosababisha aanze kuangua kilio na kutoka mbio mpaka nje ya nyumba yao iliyojengwa kwa miti na udongo na kuezekwa kwa nyasi, akakaa chini nyuma ya nyumba hiyo na kujiinamia huku akilia kwa uchungu.

Umaskini uliokithiri wa familia yao, ulikuwa ukielekea kumkosesha fursa muhimu ya kupata elimu, jambo ambalo hakuwa tayari kulikubali. Ulevi wa kupindukia wa baba yake, ulizidi kumfanya amchukie kupita kiasi kwani hata fedha kidogo alizokuwa anazipata kwa kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu, zilikuwa zikiishia kwenye vilabu vya pombe za kienyeji.
Akiwa bado anaendelea kulia kwa uchungu, alisikia sauti ya mtu akiimba kilevi, bila hata kuuliza alijua ni baba yake mzazi, Mzee Lubongeja ambaye ilikuwa kawaida yake kulewa chakari kila siku kisha kuanza kupiga kelele na kuimba nyimbo zisizoeleweka akiwa anarejea nyumbani kwake.
Kutokana na uchungu aliokuwa nao ndani ya moyo wake, Jafet hakutaka kuonana wala kuzungumza chochote na baba yake huyo, hasa muda huo akiwa amelewa. Akakimbilia kwenye kichaka kilichokuwa nyuma ya nyumba yao na kwenda kujificha, akawa anaendelea kulia kwa uchungu.
Hakuna kitu alichokuwa anakitamani kama kuendelea na masomo ya sekondari kwani kichwani alikuwa na uwezo mkubwa kiakili ndiyo maana katika shule nzima ya Rwamgasa, walifaulu wanafunzi wawili tu; yeye na mwenzake Alfayo Maguha.
Hata hivyo, kwa hali ilivyokuwa inaonesha, hakukuwa na matumaini ya yeye kuendelea na masomo ya sekondari, jambo lililosababisha alie kwa uchungu sana. Hata hivyo, kilio chake hakikuweza kubadilisha jambo lolote.
Siku hiyo ilipita, Jafet akiwa amevimba macho yaliyobadilika rangi na kuwa mekundu kutokana na kulia. Kesho yake asubuhi, mama yake aliwahi kuamka kama ilivyo kawaida yake na kuianza safari ya kwenda kufanya vibarua vya kulima mashamba ya watu ili apate chochote cha kuilisha familia yake.
“Mbona unaonekana kuwa na huzuni sana mama Jafet?”
“Mh! Mwenzangu maisha yananipeleka mbio sana, kila nikimfikiria mwanangu Jafet machozi yananitoka.”
“Kwani kuna nini tena?”
“Si unajua kwamba amefaulu kuendelea na masomo ya sekondari? Sina uwezo wa kumsomesha na mume wangu ndiyo kama hivyo tena, yeye kazi yake kulewa tu.”
“Maskini pole mwenzangu, kwa hiyo una mpango gani?”
“Sina cha kufanya, nitaendelea kumbembeleza akubaliane na ukweli kwani mimi mama yake napenda sana akasome lakini sina uwezo wa kumsomesha,” mama mzazi wa Jafet, alikuwa akizungumza na jirani yake, wakati wakiwa njiani kuelekea kwenye mashamba ya watu kufanya vibarua.
“Mimi nina wazo, nimewahi kusikia kuwa wale mapadri wa Kizungu kanisani kwetu huwa wanawasaidia vijana wenye akili kuendelea na masomo yao ili baadaye waje kuwa mapadri.”
“Wee! Kweli?”
“Ndiyo, ila masharti yao ni kwamba wakikusomesha lazima uje kuwa padri.”
“Hilo halina tatizo kabisa, kwa ninavyomjua mwanangu yupo tayari, ngoja leoleo niende maana mwanangu anavyolia mpaka ananitia uchungu,” alisema mama Jafet na kumkabidhi mwenzake jembe, hakutaka kulaza damu, muda huohuo alifunga safari kuelekea kwenye ofisi za mapadri hao zilizokuwa zimeungana na Kanisa Katoliki la Rwamgasa.
“Mbona unahema sana mama, nini tatizo?” askofu mwenye asili ya Kizungu, alimuuliza mama Jafet kwa Kiswahili kibovu baada ya kumuona akiwasili kwenye ofisi hizo huku akitweta mithili ya mwanariadha aliyetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
“Nina tatizo baba askofu.”
“Karibu sana na jisikie uko nyumbani, katika Biblia Takatifu, kitabu cha Mathayo 11:28, Yesu anasema: Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo, nami nitawapumzisha,” alisema askofu huyo kwa upole huku akimuongoza mpaka kwenye ofisi yake.
Walipoingia ndani ya ofisi ya askofu huyo, huku akilengwalengwa na machozi, mama Jafet alianza kueleza shida yake ambapo askofu huyo alikuwa akimsikiliza kwa umakini mkubwa. Baada ya kumaliza kueleza matatizo yaliyokuwa yanamsu mbua, mama Jafet alijiinamia na kuanza kutokwa na machozi.
Askofu huyo akambembeleza na kumwambia hakukuwa na sababu ya kulia kwa sababu wao walikuwa na utaratibu maalum wa kuwasomesha watoto kutoka kaya masikini lakini kwa masharti kwamba wakishahitimu masomo yao, wataingia kusomea upadri.
Mama Jafet alimshukuru sana askofu huyo na kumwambia kuwa hilo halikuwa tatizo kwa mwanaye, akamhakikishia kwamba hata akitaka muda huohuo aende kumleta ili aelezwe mwenyewe masharti yuko tayari.
“Njoo naye kesho asubuhi tuzungumze naye,” alisema askofu huyo ambaye baadaye alijitambulisha kwamba anaitwa Brocco Giovanni, mama Jafet alimshukuru sana kiasi cha kumpigia magoti, akiwa ni kama haamini kama kweli hatimaye mwanaye alikuwa anaenda kupata nafasi ya kusomeshwa na mapadri.
Hakutaka kurudi nyumbani, ilibidi aelekee kwenye kibarua chake cha kupalilia shamba la mihogo ili apate chochote cha kurejea nacho nyumbani kwa ajili ya chakula cha familia. Njia nzima wakati akielekea kibaruani, mama Jafet alikuwa akiimba mapambio na nyimbo za kumsifu Mungu kwani kilichotokea kilikuwa ni zaidi ya miujiza.
Alipofika kibaruani, alimweleza yule rafiki yake aliyemwelekeza kwenda kwa mapadri hatua aliyokuwa amefikia, akamshukuru sana na kumuombea kwa Mungu ampe maisha marefu. Siku hiyo mama Jafet alifanya kazi kwa nguvu kuliko siku nyingine zote, hakujali jua kali lililokuwa linampiga.
Hatimaye alimaliza ngwe aliyopangiwa, akalipwa mihogo na fedha kidogo kisha bila kupoteza muda, aliianza safari ya kurejea nyumbani kwake. Siku hiyo alikuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, hali iliyomfanya wala asiuone urefu wa safari ya kurejea nyumbani kwake wala jua kali lililokuwa linawaka.
Alipofika nyumbani kwake, kwenye nyumba ndogo ya nyasi na miti iliyoezekwa kwa nyasi, alimkuta mwanaye Jafet akiwa amekaa upenuni, mikono ikiwa mashavuni huku macho yake yakiwa mekundu kuonesha kwamba alikuwa analia.
“Nimekuja na habari njema mwanangu, huna haja ya kulia tena,” alisema mama Jafet, akaweka jembe lake chini na furushi la mihogo, akakaa pembeni ya mwanaye na kuanza kumsimulia kilichotokea.
“Unasema kweli mama?”
“Kweli kabisa, jiandae asubuhi tutaondoka pamoja,” alisema mama Jafet, kauli iliyomfanya kijana huyo mdogo amrukie mama yake na kumkumbatia mwilini, machozi ya furaha yakimbubujika kwa wingi.
Siku hiyo ilikuwa ya kipekee mno kwa Jafet, lile tabasamu lake la kitoto ambalo kwa muda mrefu lilikuwa limepotea, lilianza kuchanua upya usoni mwake. Akawa anasubiri kwa hamu kesho yake iwadie huku akiona kama saa zilikuwa zikienda taratibu mno.

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA