LOVE STORY 4

AKIWA kwenye ziara yake ya kikazi, mara kwa mara Rais Martin alikuwa akipiga simu ikulu kuulizia maendeleo ya mkewe ambaye alimuacha akiwa na hali ya kutatanisha.
“Mume wangu, naendelea vizuri ila nina habari njema kwako.”
“Ooh afadhali mke wangu kama unaendelea vizuri, unataka kunipa habari gani?” aliuliza Rais Martin huku akionekana kuwa na shauku kubwa.
“Wala usishtuke mume wangu kipenzi, mwenzio nime... nime...” alisema First Lady huyo lakini akashindwa kumalizia sentensi yake, akasikika akicheka kwa furaha, jambo lililozidi kumuweka Rais Martin njia panda.
“Unaniweka roho juu mke wangu, tafadhali niambie,” alisema Rais Martin huku akionesha dhahiri kuwa na shauku kubwa ndani ya moyo wake, mke wake akamwambia jambo ambalo lilimshtua na kumfurahisha mno
.
“Nimenasa ujauzito mume wangu, miezi michache ijayo na wewe utakuwa unaitwa baba,” alisema Sophia, hali iliyomlazimu mumewe kukatisha ziara muhimu aliyokuwa anaifanya.
Msafara ukageuza na kurudi ikulu huku Rais Martin akiwa bado haamini alichokuwa anakisikia. Hakuna kitu alichokuwa anakisubiri kwa hamu kama mkewe kupata ujauzito wake, jambo ambalo sasa lilikuwa limetimia.
Msafara wake ulipowasili ikulu tu, harakaharaka alishuka na kwenda moja kwa moja kwenye chumba mkewe alichokuwa amepumzika. Akaingia mbiombio na kwenda kumkumbatia huku akiachia mvua ya mabusu.
“Daktari, eti ni kweli?” Rais Martin alimuuliza daktari aliyekuwa amesimama pembeni, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akatingisha kichwa kukubali kwamba alichokuwa akiambiwa na mkewe kilikuwa kweli.
“Hongereni sana,” alisema daktari huyo kabla hajatoka na kuwapisha wawili hao walioonesha kuwa na furaha ya hali ya juu ndani ya mioyo yao. Wakakumbatiana tena na kuendelea kupongezana kwa hatua hiyo kubwa waliyokuwa wameifikia.
Siku zilizidi kusonga mbele huku ujauzito wa First Lady, Sophia ukizidi kuwa mkubwa. Kama ilivyokuwa kipindi cha ndoa yake, waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali walikuwa wakimfuatilia kwa karibu na kuripoti kuhusu maendeleo ya ujauzito wake.
Ratiba ya rais nayo ilibidi ibadilike, kazi nyingi za usiku akawa anazifanya mchana ili apate muda wa kutosha kukaa na mkewe ambaye alikuwa akideka sana kutokana na hali yake. Rais Martin aliajiri wafanyakazi wengi kuhakikisha mke wake anapewa huduma zote muhimu mpaka siku ya kujifungua itakapowadia. Mapenzi kati ya wawili hao yaliongezeka maradufu na kadiri ujauzito ulivyokuwa unazidi kuongezeka ndivyo furaha ilivyokuwa ikizidi kuchanua kwenye familia hiyo.
Hatimaye miezi tisa ilitimia, Sophia akashikwa na uchungu wa kujifungua na kukimbizwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Sangabuye ambako alilazwa kwenye wodi ya VIP, iliyokuwa na ulinzi mkali na huduma za kiwango cha juu. Akajifungua salama mtoto wa kiume.
“Whaooo! Amefanana na wewe, mtazame alivyo mzuri! Macho, pua, sura vyote kachukua vyako.”
“Mh! Mi naona kafanana na wewe, mcheki alivyo ‘handsome’, kama baba yake!” Rais Martin na mkewe walikuwa wakijadiliana na kutaniana kwa furaha ndani ya wodi ya wazazi, baada ya rais huyo kuwa mtu wa kwanza kuingia wodini na kumjulia hali mkewe pamoja na mtoto, muda mfupi tu baada ya kujifungua salama.
Habari juu ya kujifungua salama kwa mke wa rais zilisambaa kwa kasi kama moto wa nyikani, salamu za pongezi zikaanza kumiminika kama mvua ya mawe kutoka kila kona ya nchi. Wananchi wengi wakawa wanampongeza Rais Martin na mkewe kwa kupata mtoto mzuri mwenye afya njema. Vyombo mbalimbali vya habari navyo viliendelea kuripoti tukio hilo na kumfanya mtoto huyo awe maarufu akiwa bado mchanga.
“Nataka tuzae mwingine wa kike kisha ndiyo nitulie, bado hamu yangu haijaisha mpaka nitakapokuzalia mtoto wa kike, najua unampenda sana,” alisema Sophia wakiwa chumbani na mtoto wao mchanga, wazo ambalo Rais Martin alilikubali kwa haraka kwani ni kweli alikuwa akitamani sana mtoto wa kike kuliko wa kiume.
Wakakubaliana kuwa mtoto huyo atakapofikisha umri wa miaka miwili tu, wamtafutie mdogo wake. Furaha ilizidi kuongezeka kwenye familia hiyo, wakakubaliana kumpa mtoto huyo jina la Charles. Kutokana na malezi mazuri aliyokuwa akiyapata mtoto huyo, alinawiri vizuri na akawa anakua kwa kasi kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele.
Naye Rais Martin Wela alizidi kuchapa kazi ya kuitumikia nchi yake kwa uzalendo na uadilifu wa hali ya juu. Hali za kimaisha za wananchi wa Sangabuye zikawa zinazidi kuimarika kila kukicha, ule umaskini uliowatesa kwa kipindi kirefu sasa ukawa unapotea kama theluji iyeyukavyo juani.
“Hii ndiyo Sangabuye tuliyokuwa tunaitaka, tunamuombea mwanao akue haraka ili siku moja na yeye aje kuiongoza nchi yetu kama wewe baba yake ulivyofanya,” mshauri wa rais alimwambia mheshimiwa Martin Wela jioni moja wakiwa wamepumzika kwenye bustani za ikulu, rais akichezacheza na mwanaye.
Kauli hiyo ilimfurahisha sana Rais Martin, akashusha pumzi ndefu na kuanza kujadiliana na mshauri wake huyo aliyekuwa akimuongoza vyema kwenye mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiihusu nchi hiyo.
“Nafikiri sasa nchi yetu imeshatulia vizuri na huu ndiyo muda muafaka wa kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia utakaomaliza utawala wa kijeshi ulioniingiza mimi madarakani.”
“Ni kweli kabisa mheshimiwa, nadhani huu ndiyo muda muafaka wa wananchi kuamua wenyewe kwa demokrasia rais wanayemtaka ingawa najua bado chaguo lao namba moja utakuwa ni wewe.”
“Hahaaa! Hapana mimi sitagombea tena, nitawapisha wenzangu nao waoneshe uwezo walionao, mimi nitaelekeza nguvu zangu kuitunza familia yangu kwa sababu nikiwa hapa ikulu nakosa uhuru wa kutosha wa kukaa na familia yangu.”
“Wananchi hawatakubali kabisa, yaani ni bora uendelee kuongoza wewe kijeshi kuliko kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia halafu usigombee. Mimi siwasemei wananchi lakini amini nakwambia bado wanakuhitaji sana,” alisema msaidizi huyo wa rais, wakaendelea kuzungumza mambo mbalimbali lakini bado Martin alionesha kutokuwa na nia ya kugombea tena urais.
Siku chache baadaye, Rais Martin Wela aliwahutubia wananchi wa Sangabuye ambapo mbali na mambo mengine, alitangaza nia yake ya kuirejesha nchi hiyo katika mfumo wa kiraia baada ya yeye kuiongoza kwa muda, akiwa amewekwa madarakani na jeshi.
Taarifa hiyo ilipokelewa kwa mikono miwili na wananchi wengi ambao walipendekeza kuwa Rais Martin agombee kupitia mfumo wa kidemokrasia kwa sababu bado wananchi wengi walikuwa wakihitaji aendelee kuwaongoza.
“Naona mheshimiwa umeamini mwenyewe, unaona watu wanavyotoa maoni yao kuhusu mpango wa kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia? Wewe ndiyo nyota ya Sangabuye, una mvuto wa kipekee kwa jamii na hakuna anayeweza kushindana na wewe,” mshauri wa rais alimweleza Martin wakiwa wamekaa kwenye ofisi ya rais, ikulu wakifuatilia mahojiano ya watu mbalimbali waliokuwa wakitoa maoni yao kuhusu uchaguzi wa kidemokrasia.
Ilibidi Martin arudi kwa uongozi wa juu wa jeshi ambao ndiyo uliomuweka madarakani, akawaeleza kwamba hafikirii kugombea tena kwa sababu atakuwa bize na ulezi wa familia yake, wazo ambalo lilipingwa vikali na viongozi hao waliomtaka kugombea ili aendelee na kazi nzuri aliyokuwa ameianza.
Martin hakuwa na ujanja, ilibidi afanye kama alivyokuwa ameelekezwa, mchakato wa kuunda serikali ya kidemokrasia ukaanza ambapo vyama mbalimbali vya siasa vilianza kusajiliwa upya. Martin Wela akaunda Chama cha Sangabuye Alliance for Democracy and Transparency (SADT)

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA