LOVE STORY 3

Ebola, ugonjwa usio na tiba wala kinga umeikumba nchi ya Liberia na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wake. Watu wengi wanaambukizwa ugonjwa huo na ndani ya muda mfupi tu, mamia ya wananchi wanapoteza maisha. Hali ya hatari inatangazwa nchi nzima ambapo maeneo yaliyoathirika zaidi yanawekwa chini ya karantini maalum, watu wakizuiwa kuingia au kutoka bila kuwa na sababu maalum.
Licha ya serikali iliyokuwa inaongozwa na rais mwanamke, mwanamama shupavu mwenye moyo wa kipekee,  Hellen Joseph, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kupambana na ugonjwa huo, kazi inakuwa ngumu na maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha na kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Hali inazidi kuwa tete kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, maiti nyingi za watu waliokufa kwa ugonjwa huo zinatapakaa mitaani huku maelfu ya wakazi wakiyakimbia makazi yao wakiogopa kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Jiji la Monrovia linabaki kuwa kimya kabisa huku harufu za maiti zikizidi kuifanya hali kuwa ya kutisha mno. Mitaa yote inakuwa kimya kabisa, kelele pekee zinazosikika ni za mbwa wanaogombea mizoga ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo.
Ndani ya nyumba moja, watu wawili waliokuwa wapenzi wanasikika wakibishana. Mwanaume anamtaka mpenzi wake aondoke na kurudi nchini kwao, Sangabuye ili asije akaambukizwa ugonjwa huo lakini mwanamke anakataa akitaka waondoke pamoja au wabaki wote na kufa pamoja.
Upande wa pili, historia ya nchi ya Sangabuye inamulikwa ambapo Rais Martin Wela anaingia madarakani baada ya serikali iliyokuwepo kupinduliwa. Kwa kuwa Martin alikuwa bado hajaoa, anapewa ushauri wa kutafuta mke na kura yake inamuangukia mpenzi wake wa siku nyingi, Sophia Marcel. Mipango ya ndoa inaanza kufanyika.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Maandalizi yote muhimu kuelekea kwenye ndoa ya kipekee kati ya Rais Mteule wa Sangabuye, Martin Wela na mwanamke mrembo kuliko wote, mrefu kama twiga, aliyejaaliwa umbo lenye mvuto wa aina yake, Sophia Marcel, yalizidi kupamba moto.
“Siamini kama unaenda kuwa mume wangu Martin, siamini,” Sophia alimwambia mpenzi wake huyo wa muda mrefu waliyedumu pamoja kwenye shida na raha mpaka kufikia hatua ya kutorokea mafichoni wakikwepa kukamatwa na serikali kutokana na itikadi za kiuanaharakati alizokuwa nazo Martin.
“Wewe ndiyo mwanamke wa maisha yangu, umenivumilia kwa muda mrefu sana Sophy, nakupenda sana na naahidi kukupenda maisha yangu yote,” alisema Rais Martin na kumbusu Sophia kwenye shavu lake, akamkumbatia kimahaba, jioni ya siku moja kabla ya ndoa yao iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa.
“Kwa hiyo na mimi nitakuwa first lady? Na mimi nitakuwa naishi ikulu?”
“Ndiyo Sophy, kama uliweza kuishi na mimi uhamishoni kwa nini isiwezekane kuishi ikulu? Huu ni wakati wetu wa kuwatumikia watu wa Sangabuye na kurejesha imani yao kwa serikali, naamini utakuwa mshauri mzuri kwangu kama ambavyo siku zote umekuwa.”
“Ahsante sana mpenzi wangu, nitakupenda daima Martin,” alisema Sophy kisha wakakumbatiana tena. Waliendelea kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu maisha yao ya baadaye, wakiwa wamekaa kwenye viunga vya ikulu, kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.
Hatimaye siku ya harusi iliwadia, viunga vyote vya ikulu kuanzia kwenye bustani za nje mpaka ndani kukapambwa na wapambaji maalum waliokodiwa maalum kwa ajili ya kazi hiyo na kuifanya Ikulu ya Sangabuye kubadilika mno.
Wageni wengi maarufu walialikwa, wakiwemo marais wa nchi jirani, viongozi wa juu wa taasisi mbalimbali za kimataifa, viongozi wa majeshi ya nchi mbalimbali na vigogo wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Hatimaye Martin akafunga ndoa ya kifahari iliyohudhuriwa na wageni wengi mashuhuri na kuweka historia ya kipekee katika historia ya maisha yake. Kutokana na jinsi alivyokuwa akikubalika miongoni mwa wananchi wa Sangabuye, ndoa hiyo ilivuma mno.
Kila redio, runinga, magazeti na mitandao vikawa vinaripoti tukio hilo huku watu wengi wakikata vipande vya magazeti vilivyokuwa na picha za maharusi hao na kubandika kwenye vyumba vyao kama kumbukumbu.
Furaha kubwa zaidi ilikuwa kwa Martin mwenyewe na mkewe mpya, Sophia ambao kwa pamoja walionesha kuwa na raha za ajabu ndani ya mioyo yao kwani ndoa hiyo waliisubiri kwa kipindi kirefu na sasa hatimaye ilikuwa imetimia.
Baada tu ya ndoa kuisha, Rais Martin na mkewe walisafiri kwa ndege maalum mpaka Comoro walikokaa kwa siku saba wakila fungate. Waliporudi, kila mmoja alikuwa mpya kabisa, wakiwa mume na mke halali.
“Sasa umekamilika mheshimiwa rais, unaweza kuendelea na majukumu yako kama kawaida,” mshauri wa rais alimwambia bosi wake wakiwa kwenye ofisi yake, siku moja tangu arejee kutoka fungate.
Wote wakacheka na kugongesheana mikono kwani mshauri huyo ndiye aliyempa wazo la kufunga ndoa kabla hajaanza rasmi kazi ya kuiongoza Sangabuye. Siku hiyo ilipita, Rais Martin akaendelea kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuhakikisha anaiongoza vyema nchi hiyo.
Mageuzi makubwa yakaanza kufanyika ambapo mfumo wa ujamaa ambao ndiyo uliokuwa ukitumika kwa kipindi kirefu tangu nchi hiyo ilipopata uhuru, ulianza kufutwa hatua kwa hatua. Viwanda vingi vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali vilibinafsishwa kwa wazawa ambao walikuwa wakiingia mikataba na wawekezaji wa nje ya nchi katika kuviboresha.
Leseni za kuanzisha viwanda vingine vipya nazo zikawa zinatolewa kwa wingi huku mara kwa mara rais huyo kijana na mchangamfu akiwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi bila woga na kuzitumia vizuri fursa zilizokuwa zikipatikana.
Ndani ya kipindi kifupi tu, viwanda vingi vilivyobinafsishwa vilipanuliwa na kuongezwa ufanisi ambapo sasa bidhaa nyingi zilianza kuzalisha ndani ya mipaka ya Sangabuye.
Wananchi wengi ambao awali walikuwa wakitegemea kilimo kama uti wa mgongo, sasa wakaajiriwa viwandani ambako walikuwa wakilipwa mishahara mikubwa tofauti na vipato walivyokuwa wanapata kupitia kilimo.
Taratibu maisha ya kila mwananchi yakaanza kubadilika, bei ya bidhaa mbalimbali ikashuka madukani kutokana na viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa nyingi na serikali kuvipunguzia kodi, kila mtu akawa anayaona mabadiliko ya waziwazi yaliyokuwa yanatokea.
Mabadiliko yaliendelea kupamba moto, vijana wengi na wanawake wakawa wanapewa elimu ya ujasiriamali ambayo iliwafanya wengi kujiajiri na kuwaajiri wengine huku mikopo iliyokuwa ikitolewa na serikali na taasisi nyingine za kifedha kwa riba nafuu ikizidi kurahisisha maisha ya wengi.
“Mume wangu wewe ni kiongozi mzuri sana, najivunia kuwa na mume mzuri kama wewe,” Sophia alimwambia mumewe wakiwa ikulu, asubuhi moja wakati akimuandaa kuelekea kwenye ziara ya kikazi sehemu mbalimbali za Sangabuye.
“Kwa nini unasema hivyo mke wangu?”
“Umeyabadilisha sana maisha ya Sangabuye, yaani laiti kama baada tu ya kupata uhuru tungekupa wewe jukumu la kutuongoza huenda leo tungekuwa tunakaribiana na Marekani kwa maendeleo.
“Ndani ya muda mfupi tu umebadilisha mno maisha ya wananchi wa...” Sophia hakumalizia sentensi yake, ghafla akajishika mdomoni na kutoka mbio mpaka kwenye sinki lililokuwa kwenye korido ya ikulu.
Rais Martin Wela alishtuka mno kumuona mkewe akiwa kwenye hali hiyo, akaacha kila kitu na kumkimbilia pale kwenye sinki alipokuwa amejiinamia, akazidi kupatwa na hofu baada ya kugundua kumbe mkewe alikuwa akitapika.
“Pole mke wangu, umepatwa na nini?” alisema Martin huku akimshika mkewe kwa upole na kumsaidia kuinuka. Akafungulia maji na kumnawisha kisha akambeba kwenye mikono yake na kumrudisha mpaka sebuleni, akamlaza kwenye sofa la kifahari huku akitoa simu yake na kuwapigia wasaidizi wake waliokuwa ndani ya jengo hilohilo.
Harakaharaka wanawake wanne waliokuwa wakifanya kazi ya kumlinda mke wa rais wakaingia na kwenda mpaka pale mke wa Rais Martin alipokuwa amelazwa. Akawaeleza kilichotokea na kuwataka wahakikishe wanamsaidia haraka.
Daktari wa rais akapigiwa simu haraka huku wale wanawake waliokuwa wamevalia mavazi maalum wakiendelea kumpa huduma ya kwanza Sophia. Japokuwa muda wa kuondoka ulikuwa umefika na tayari msafara wa rais ulikuwa tayari nje ya ikulu, Rais Martin hakuweza kutoka mpaka ajue nini kilichokuwa kinamsumbua mke wake.
Muda mfupi baadaye, daktari aliwasili akiwa na vifaa vyote muhimu, harakaharaka akaanza kumpima Sophia aliyekuwa ametulia kwenye sofa, huku akiendelea kulalamika kusikia kichefuchefu. Baada ya kumpima vipimo vyote vya msingi, daktari huyo hakubaini tatizo lolote, akamruhusu Rais Martin aendelee na kazi zake wakati yeye akiendelea kumchunguza mgonjwa taratibu.
“Hakikisha anakuwa sawa daktari, tafadhali msaidie mke wangu,” alisema Rais Martin na kumbusu mkewe kisha akatoka nje ambako msafara wake ulikuwa ukimsubiri. Akaingia kwenye gari lake na safari ya kwenda kuwatembelea wananchi wa sehemu mbalimbali na kusikiliza matatizo yao ikaanza.
Je, nini kitafuatia? Mke wa rais anataka kumpa habari gani mumewe? Usikose hatua inayofuata

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA