LOVE STORY

“Natangaza hali ya hatari, nchi yetu imekumbwa na balaa kubwa. Sote tutakuwa mashahidi wa jinsi ndugu zetu wa karibu, familia zetu, watu tunaowapenda na majirani zetu wanavyozidi kupukutika kutokana na ugonjwa huu
wa ajabu uliotukumba.
“Natangaza hali ya hatari, watu wasiruhusiwe kutoka au kuingia kienyeji ndani ya mipaka ya nchi yetu bila kupimwa. Kwa wale watakaothibitika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huu, haraka wapelekwe kwenye vituo maalum vilivyotengwa kwa ajili ya kazi hii.
“Pia nichukue fursa hii kuwapongeza wa hudumu wa afya, manesi na madaktari wa  nchi nzima ambao mmejitolea kadiri ya uwezo wetu, mkiyaweka maisha yenu hatarini kwa ajili ya kupigania maisha ya wengine kama mlivyokula kiapo.
“Serikali inafanya kila kinachowezekana kuhakikisha mnapatiwa vifaa vya kujikinga ili msipate maambukizi kama ilivyotokea kwa baadhi ya wenzenu. “Nayatangaza maeneo ya Mji wa Dolo, Bomi, Bong, Grand Bassa, Grand Cape Mount, Lofa, Margibi, Montserrado, Nimba, Mto Cess na jiji lote la Monrovia kuwa chini ya karantini maalum.
“Wanausalama wote fanyeni kazi yenu kwa kushirikiana na watumishi wa wizara ya afya kuhakikisha hakuna anayeingia wala kutoka kwenye maeneo niliyoyataja,” Rais wa Liberia, Hellen Joseph, mwanamke wa kwanza kuiongoza nchi hiyo katika historia, alikuwa akilihutubia taifa katika hotuba ya dharura kufuatia kuibuka kwa ugonjwa hatari wa Ebola uliolitingisha vibaya taifa hilo.
Kila mtu alikuwa kimya, wengine wakiwa kando ya redio zao, wengine pembeni ya televisheni zao wote wakisikiliza hotuba hiyo kutoka kwa rais wao aliyekuwa akihutubia kupitia Shirika la Utangazaji la Liberia (Liberia Broacasting System).
Utekelezaji wa alichokiagiza ukaanza kufanyika haraka ambapo miji yote iliyotajwa iliwekwa kwenye karantini, ikiwepo makao makuu ya nchi hiyo, Monrovia. Ikawa hakuna mtu aliyekuwa anaruhusiwa kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine bila kuwa na sababu ya msingi.
Hata wale waliokuwa na ulazima wa kusafiri kuingia au kutoka kwenye maeneo yaliyowekewa karantini, walikuwa wakipimwa afya zao kabla ya kuruhusiwa kusafiri.Licha ya tahadhari kubwa zilizokuwa zinachukuliwa na serikali kupitia wizara ya afya na taasisi nyingine, bado kasi ya maambukizi ilizidi kushika kasi katika nchi hiyo iliyopo Afrika Magharibi. Mamia ya watu wakawa wanaambukizwa kila kukicha na kukimbizwa kwenye vituo maalum ambavyo vilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Wahudumu wa afya waliokuwa wakivaa mavazi maalum yaliyofunika miili yao yote, kuanzia juu hadi chini, waliendelea kufanya kazi usiku na mchana huku wengine wakipita kwenye makazi ya wananchi na kuwaeleza dalili za ugonjwa huo na namna ya kujikinga.
Taasisi ya Planet Link Health Care iliyokuwa na makao makuu yake nchini Marekani katika Jiji la California, Texas, nayo ilituma wataalamu wake nchini Liberia kwa ajili ya kwenda kuwaelimisha wananchi juu ya maana ya ugonjwa huo, dalili zake, jinsi unavyoambukizwa na namna ya kuuzuia.
“Ugonjwa huu unasambazwa na virusi viitwavyo Ebola Virus ambavyo husambazwa kwa kugusa mwili wa mgonjwa, damu, mate au majimaji ya mwilini, zikiwemo mbegu za kiume.
“Kwa mara ya kwanza, ugonjwa huu uligundulika kwenye miili ya sokwe na popo waliokuwa wakipatikana kandokando la Mto Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan mwaka 1976 na ukahamia kwa binadamu ambako umeendelea kusambaa kwa kasi kubwa mpaka kufika hapa nchini Liberia.
“Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa kali ya ghafla, maumivu makali ya kichwa, kutokwa damu kwenye viungo mbalimbali vya mwili, kutapika, kuhara na mwili kukosa nguvu na dalili hizo huanza kuonekana siku mbili baada ya mtu kuambukizwa.
Asipopata tiba ya haraka, hufa ndani ya saa zisizozidi sita.
“Ukiigusa maiti ya mtu aliyekufa kwa Ebola au kuikaribia, nawe utaambukizwa ndani ya muda mfupi. Wagonjwa wa Ebola ni lazima watengwe ili wasiwaambukize wenzao na ni makosa makubwa kumgusa mgonjwa wa Ebola kwani lazima nawe utaambukizwa.
“Dalili za mwishomwisho kabla ya mgonjwa wa Ebola kufa ni kutapika damu, kukohoa makohozi yenye damu na kuharisha damu. Pia kutokwa na damu puani, mdomoni na masikioni.
“Ni lazima maiti za watu waliokufa kwa Ebola zizikwe na wataalamu wa afya kwa kuzingatia kanuni maalum ikiwemo kuchimba kaburi refu na kumwagia madawa ya kutosha kwenye makaburi,” wataalamu wawili wa shirika la Planet Link Health Care, walikuwa wakitoa semina maalum kwa wananchi, kupitia redio na televisheni ya taifa.
Hata hivyo, elimu hiyo muhimu ilikuja kwa kuchelewa kwani tayari kasi ya maambukizi ya Ebola ilikuwa imepamba moto, vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hao vilionekana kuzidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa, hali ikazidi kuwa tete.
Ilibidi hospitali zote kubwa jijini Monrovia, nazo zianze kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola. Hospitali za John F. Kennedy Medical Center, Eternal Love Winning Africa,     Redemption, St. Joseph’s Catholic, Seven Days Adventist, MSF Pediatric, E.S. Grant Mental Health, A.M.E. University Clinic na nyingine nyingi zote zilifurika wagonjwa wa Ebola.
Licha ya jitihada za madaktari na manesi, bado hali ilizidi kuwa tete, wagonjwa wakazidi kufa na kibaya zaidi, hata madaktari waliokuwa wakiwahudumia, nao walianza kuambukizwa ugonjwa huo hatari ambao mpaka muda huo, haukuwa na tiba ya uhakika.
Kitendo cha madaktari kuanza kuugua na kufa, kilizidi kuifanya kazi iwe ngumu kwani wengine waliogopa na kuanza kukimbia mmoja baada ya mwingine kuokoa maisha yao. Madaktari wachache ambao kweli walikuwa wakizingatia weledi wa kazi zao, wao waliendelea na kazi.
ataifa ya kigeni ambayo yalikuwa na raia wao kwenye nchi hiyo, nayo yalianza kuwahamisha na kuwarudisha makwao baada ya kuwapima na kuthibitika kwamba hawakuwa na ugonjwa huo. Ofisi za mabalozi wa nchi zote zikafungwa na kila mtu akaja kuchukuliwa na nchi yake kurudishwa nyumbani kwao.
Siku tano baadaye tangu rais alipotangaza hali ya hatari, vifo vya wagonjwa wa Ebola vilikuwa vimeongezeka zaidi ya mara kumi ukilinganisha na awali, maiti nyingi zikawa zinazagaa mitaani na kusababisha Jiji la Monrovia na vitongoji vyake kutawaliwa na harufu za wafu.
Licha ya maagizo ya serikali kuwazuia watu kutotoka wala kuingia kwenye maeneo yaliyokuwa chini ya karantini, maelfu ya watu waliyakimbia makazi yao wakihofia kufa na ugonjwa huo, mitaa ikabaki kimya kabisa. Kelele pekee zilizokuwa zinasikika, zilikuwa ni za mbwa waliokuwa wakifaidi mizoga ya binadamu waliokufa kwa ugonjwa huo wa Ebola.
“Baby, go back to Sangabuye, please go baby!” (Mpenzi, tafadhali rudi Sangabuye, tafadhali nenda mpenzi)“I’m not going anywhere, if you want me to leave, we must go together otherwise let me die with you.” (Siendi popote, kama unataka niondoke lazima tuondoke pamoja vinginevyo niache nife na wewe)“But baby, you know I’m a doctor and I’m devoted to my career, I can’t leave here and let my patients die helpless.
(Lakini mpenzi, unajua kwamba mimi ni daktari ambaye nimejitolea maisha yangu yote kwa ajili ya kazi yangu, siwezi kuondoka na kuwaacha wagonjwa wangu wakifa bila msaada).
Watu wawili walikuwa wakibishana kutoka ndani ya nyumba moja iliyokuwa katikati ya Jiji la Monrovia. Mazungumzo yao yaliendelea kwa muda mrefu lakini muafaka haukufikiwa, licha ya mwanaume kumsisitiza mpenzi wake huyo aondoke ili asije akaambukizwa ugonjwa huo hatari, mwanamke hakuwa tayari.
Akawa anamng’ang’ania waondoke pamoja ili kama ni kunusurika, wanusurike wote kuliko kuondoka peke yake kwani alikuwa anajua nini kingetokea endapo angeondoka na kumuacha mpenzi wake huyo ambaye walikuwa kwenye hatua za mwisho za kufunga ndoa kabla ya kulipuka kwa ugonjwa huo.
Je, nini kitafuatia? Wapenzi wanaobishana ndani ya chumba hicho ni nani na nani? Nini hatima ya nchi ya Liberia na ugonjwa wa Ebola? Usikose

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA