LOVE STORY 2

Ugonjwa wa kutisha usio na tiba wala kinga, Ebola umeikumba nchi ya Liberia na kusababisha maafa makubwa. Hali ya hatari inatangazwa nchi nzima ambapo maeneo yaliyoathirika sana yanawekwa chini ya karantini maalum, watu wakizuiwa kuingia au kutoka bila kuwa na sababu maalum.
Licha ya serikali iliyokuwa inaongozwa na rais mwanamke, mwanamama shupavu mwenye moyo wa kipekee,  Hellen Joseph, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kupambana na ugonjwa huo, kazi inakuwa ngumu na mamia ya watu wanaendelea kupoteza maisha na kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Hali inazidi kuwa tete kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, maiti nyingi za watu waliokufa kwa ugonjwa huo zinatapakaa mitaani huku maelfu ya wakazi wakiyakimbia makazi yao wakiogopa kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Jiji la Monrovia linabaki kuwa kimya
kabisa huku harufu za maiti zikizidi kuifanya hali kuwa ya kutisha mno. Mitaa yote inakuwa kimya kabisa, kelele pekee zinazosikika ni za mbwa wanaogombea mizoga ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo.
Ndani ya nyumba moja, watu wawili waliokuwa wapenzi wanasikika wakibishana. Mwanaume anamtaka mpenzi wake aondoke na kurudi nchini kwao, Sangabuye ili asije akaambukizwa ugonjwa huo lakini mwanamke anakataa akitaka waondoke pamoja au wabaki wote na kufa pamoja.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Tafadhali mpenzi wangu, naomba unielewe Rafiki, rudi nyumbani mpenzi wangu, mimi nikimaliza tu kazi nitakuja.”
“Hapana Lawrence, siwezi kuondoka na kukuacha. Ni juzi tu tumesherehekea pamoja Sikukuu ya Krismasi hapa Monrovia kabla Ebola haijalipuka, leo unataka niondoke na kukuacha peke yako? Umesahau nini kipo mbele yetu?”
“Sijasahau Rafiki mpenzi wangu, najua siku chache baadaye tutafunga ndoa na kuwa mume na mke halali baada ya kusubiri kwa muda mrefu lakini hii kazi ninayoifanya ni muhimu sana.”

Unataka kusema kutibu wagonjwa wa Ebola ni muhimu kuliko mimi na wewe kufunga ndoa? Lawrence mpenzi wangu, zimebaki wiki mbili tu kabla hatujafunga ndoa leo unataka niondoke na kukuacha. Ukifa je?”
“Siwezi kufa Rafiki mpenzi wangu, nitajitahidi kuwa makini.”
“Huwezi kufa? Umeshuhudia mpaka sasa madaktari wangapi wamekufa? Kwani wao hawakuwa makini?”
“Hapana Rafiki, nakuomba tafadhali nielewe, rudi nyumbani mimi nitakuja siku chache zijazo. Ndugu zako, familia yako na watu wote watanichukia sana endapo utapatwa na Ebola kwani watajua mimi ndiyo chanzo kwa sababu wanajua umenifuata mimi huku Liberia.”
“Kumbe hunipendi Lawrence, nimegundua kwamba nalazimisha mapenzi kwako wala hunipendi,” alisema msichana huyo huku akianza kuangua kilio kama mtu aliyepokea taarifa za msiba.

Lawrence akasimama dirishani na kutazama nje, maiti nyingi za wagonjwa wa Ebola zikiwa zimezagaa kila sehemu na kuifanya hali iwe ya kutisha mno. Akamgeukia Rafiki aliyekuwa amekaa kwenye kochi dogo, akiendelea kulia kwa kwikwi kiasi cha kuufanya uso wake ubadilike rangi na kuwa mwekundu. Akajikuta akibaki njia panda, akishindwa kuamua nini cha kufanya.
* * *
Kutokana na hali mbaya iliyokuwa inaendelea kulitingisha taifa la Liberia, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) ilibidi liingilie kati kwa kutangaza hali ya hatari duniani kote kwamba watu hawatakiwi kabisa kuvuka mipaka ya Liberia na kuingia kwenye nchi hiyo kwa sababu ya ugonjwa huo.
Safari zote za ndege zilizokuwa zikiingia kwenye nchi hiyo zilifutwa mara moja na kuwaacha mamia ya abiria wakisuasua kwenye viwanja mbalimbali vya ndege. Shirika hilo pia lilituma timu ya madaktari wake wengi waliokuwa na vifaa vya kisasa zaidi vya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwenda kutoa msaada kwa madaktari wa Liberia walioonesha kuzidiwa na kazi hiyo.
Ndege maalum zikasafiri zikiwa na madaktari, vifaa, madawa na vitu vyote muhimu kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo na baada ya kusafiri kwa saa nyingi angani, hatimaye zilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Roberts International Airport (Zamani Robertsfield).
Madaktari hao walipokelewa na wenzao wa Liberia na kupelekwa moja kwa moja mpaka kwenye Hospitali Kuu ya Monrovia (JFK) ambayo ndiyo ilikuwa kambi kubwa ya madaktari waliokuwa wakihaha kupambana na Ebola na muda mfupi baadaye, walianza kazi ya kuhakikisha wanapambana na Ebola.
* * *
Jamhuri ya Sangabuye, ilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zikipatikana katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ikipakana na nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Zambia na Malawi huku upande wa Mashariki, ikiwa imepakana na Bahari ya Hindi.
Baada ya kudumu kwenye siasa za chama kimoja kwa kipindi kirefu, huku rais wake akisimamia mfumo wa ujamaa ambao ulikuwa ukipingwa na watu wengi, nchi hiyo ilijikuta ikiingia kwenye machafuko makubwa baada ya watu waliokuwa wanapinga mfumo wa ujamaa kuanza kuizidi nguvu serikali.
Martin Wela alikuwa ni  mwanaharakati ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa adui namba moja wa serikali iliyokuwa madarakani kutokana na msimamo wake wa kumtaka rais kuachana na mfumo huo kwani haukuwa na tija yoyote.
Badala yake, Martin Wela alishauri utumike mfumo wa kibepari ili kuleta maendeleo ya haraka na kuwakomboa wananchi wa Sangabuye waliokuwa wanateseka na umaskini uliokithiri. Misimamo yake ilimfanya kujulikana sana ndani na nje ya nchi huku wananchi wengi wa Sangabuye wakimuunga mkono na kumuona kama mkombozi wao wa kweli.
Hata wakati vurugu za kuukataa mfumo wa ujamaa zilipopamba moto, Martin Wela ambaye alikuwa akiishi uhamishoni kutokana na hofu ya kuuawa na wafuasi wa rais wa nchi hiyo, alikuwa akitajwa na wananchi wengi kwamba ndiye anayefaa kuingia madarakani kuiongoza nchi hiyo.
Vurugu zilipozidi, Jeshi la Wananchi wa Sangabuye liliamua kuchukua nchi kwani serikali iliyokuwepo, ilionekana kushindwa kabisa kukabiliana na wananchi wake.
Kwa kuwa hata viongozi wa juu wa jeshi walikuwa wakimfahamu vizuri Martin Wela na kukubaliana na harakati zake, walikubaliana kwamba ndiyo apewe jukumu la kuiongoza nchi kwa usaidizi wa karibu wa jeshi hilo.
Martin aliyekuwa mafichoni nchini Rwanda, akafuatwa na maafisa wa jeshi hilo na kurudishwa mpaka Sangabuye ambapo siku mbili baadaye, alitangazwa na jeshi kuwa rais mpya wa nchi hiyo mpaka uchaguzi wa kidemokrasia utakapoitishwa.
Wananchi wengi waliipokea taarifa hiyo kwa shangwe kubwa, vigelegele na shangwe za kila aina zikawa zinasikika kila sehemu ya nchi hiyo huku kila mmoja akiwa na imani kubwa juu ya rais huyo mpya ambaye licha ya umri wake mdogo wa miaka 26 tu, alionekana kuwa na busara za hali ya juu.
Rais huyo mpya akavunja rekodi ya kuwa rais mdogo zaidi duniani, huku akipewa jukumu kubwa la kuipitisha nchi hiyo katika mageuzi makubwa ya kiitikadi kutoka ujamaa hadi ubepari na kisiasa kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja hadi wa vyama vingi ambao ulionekana kuwa kielelezo cha demokrasia ya kweli.
Martin Wela aliyaanza maisha mapya akiwa rais wa nchi hiyo, baada ya kuwa amehangaika kwa kipindi kirefu, akikamatwa, kuteswa na kupigwa na polisi, akitishiwa kuuawa na kujeruhiwa kwa risasi mara kadhaa mpaka alipofikia hatua ya kukimbilia uhamishoni.
“Ili uiongoze nchi vizuri, ni lazima uwe na mke mheshimiwa rais,” mshauri mkuu wa rais, Alfred Msole alimwambia rais siku chache baada ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo, wazo ambalo hata yeye alilikubali haraka kwani tayari alikuwa na mchumba wake wa siku nyingi, waliyekutana wakiwa masomoni.
Sophia Marcel, mwanamke mrembo kuliko wote nchini Sangabuye, aliyekutana na Martin Wela wakiwa masomoni nchini Uingereza ndiye aliyekuwa chaguo la rais huyo kijana kuliko wote. Kwa kuwa naye alikuwa mafichoni kwa kipindi chote hicho pamoja na mchumba wake huyo, taratibu za kumfuata nchini Rwanda zilifanyika haraka na siku chache baadaye, akaletwa ikulu.
Harakaharaka mipango ya harusi ikaanza kupangwa huku uzuri wa mwanamke huyo, ukiwa gumzo kubwa miongoni mwa wananchi wa Sangabuye.
“Anastahili kabisa kuwa mke wa rais, unamuona jinsi alivyo mzuri! Mtoto mrefu kama twiga, mtazame alivyoumbika vizuri sehemu za nyuma na kifuani, dah! Kweli rais wetu anajua kuchagua,” vijana wawili waliokuwa wakifuatilia habari juu ya ndoa hiyo kwenye runinga, walikuwa wakijadiliana na kucheka kwa furaha.
Mipango ilizidi kupamba moto, kwa jinsi rais huyo alivyokuwa akipendwa na wanachi wake, wengi walijitokeza kumuunga mkono kwa hali na mali kuhakikisha harusi hiyo inakuwa ya kihistoria.
Hatimaye maandalizi yote yalikamilika na kilichokuwa kikisubiriwa, ilikuwa ni siku ya tukio kufika. Kila mtu akawa na shauku kubwa ya kumuona rais mpya, Martin Wela akimvalisha pete mwanamke mrembo kuliko wote, Sophia Marcel.
Je, nini kitafuatia?

Comments

Popular posts from this blog

TUMIA SMS HIZI KUBORESHA PENZI LENU

FAIDA TISA ZA MBEGU ZA MABOGA KATIKA MWILI WA BINADAMU

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA